Habari

Msako mkali wa pombe haramu wafanywa Githurai 

September 11th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MSAKO mkali dhidi ya pombe haramu katika mtaa wa Githurai 44, Kaunti ya Nairobi na Githurai 45 umeanzishwa.

Shughuli hii ilianza mnamo wikendi, watengenezaji wa chang’aa na baa na vilabu vinavyouza pombe ambayo haijatathminiwa na kupitishwa na shirika la ubora wa bidhaa nchini, Kebs, wakilengwa.

Jumatatu, maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kimbo, Ruiru, walifanya operesheni katika mabaa kadhaa Githurai 44.

“Baadhi ya mabaa yenye leseni yanauza pombe haramu, ni hatia na hatutaruhusu hilo kufanyika,” mmoja wa maafisa walioshiriki msako huo na aliyeomba tusichapishe jina lake aliambia Taifa Leo.

Baa nyingi zimekiuka sheria maarufu kama za Mututho ambapo zinafunguliwa mchana.

Wakati akihudumu kama mwenyekiti wa shirika la kudhibiti utumizi wa dawa za kulevya na vileo, Nacada, aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho aliasisi sheria kukabiliana na pombe, mojawapo ikiwa baa zifunguliwe saa kumi na moja jioni.

“Baa eneo hili zinahudumu mchana peupe. Isitoshe, nyingi zinauza pombe haramu na hatari,” alilalamika mkazi.

Kukamata

Na kwenye operesheni ya Jumanne, baadhi ya wahudumu na waraibu wa vileo walikamatwa.

Kulingana na OCS wa Kimbo, Hassan Pole, katika mtaa wa Githurai 45 watengenezaji kadhaa wa chang’aa wametiwa nguvuni.

Progressive, Mumbi na Mwihoko, yametajwa kama maeneo yaliyoathirika pakubwa.

Baada ya kuchaguliwa, Gavana wa Kiambu 2017, afisi ya Ferdinand Waititu ilitwaa wajibu wa kutoa leseni za baa.

Bw Waititu alidai maafisa wa polisi katika kaunti hiyo wameshindwa kudhibiti uuzaji na unywaji wa pombe haramu.

Kiambu ni mojawapo ya kaunti zilizoathirika pakubwa na kero ya pombe haramu na hatari.