Makala

Msako wa Pombe: Wahudumu wa teksi walia kukosa wateja usiku

March 17th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

WAHUDUMU wa teksi jijini Nairobi sasa wametoa malalamishi kwamba operesheni kali ya serikali kudhibiti biashara ya pombe nyakati za usiku imechangia pakubwa kupungua kwa wateja, ambao wengi huwa ni walevi wakienda au wakitoka vilabuni.

Bw Nathan Kamau ambaye ni dereva wa teksi jijini, aliambia Taifa Jumapili kwamba kabla ya operesheni hiyo, kazi ya teksi ilikuwa ikiwaingia kipato kizuri.

Lakini sasa kwa idadi ya wateja kupungua, analazimika kufanya kazi hadi mwendo wa saa tatu za usiku.

“Kazi yetu ilikuwa ikitegemea wanywaji wa pombe wakati wa usiku. Siku ya Ijumaa ningelala mchana kutwa nikijua usiku ningefanya kazi ya maana kufidia saa za mchana,” akasema Bw Kamau.

Vita dhidi ya pombe haramu na kukabiliana na wauzaji wa pombe wasiotii sheria vimechangia vituo vingi vya burudani kufungwa, wamiliki wengi wakihofia kukamatwa na polisi.

“Nilikuwa napeleka mteja kutoka Kilimani kuelekea Roysambu kisha napata ombi la mteja mwingine kutoka Roysambu nimpeleke mitaa ya Eastlands. Usiku kucha–kuanzia saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi siku inayofuatia–nilikuwa niko kazini,” akaongeza dereva huyo.

Naye Bi Catherine Maina ambaye ni mwanamke dereva wa teksi, aliambia Taifa Jumapili, ushindani nyakati za mchana umeongezeka, na sasa mapato yamekuwa ni kidogo.

“Wakati niliingia kwa hii biashara, hakukuwa na ushindani mkubwa. Lakini sasa mbali na operesheni dhidi ya baa na vilabu, pia program za huduma za teksi zimekuwa nyingi. Sasa hivi madereva pia ni wengi na kila mtu anang’ang’ania kupata riziki yake mchana,” akasema Bi Maina.

Hali hiyo imepelekea wahudumu hao kuhofia kufanya kazi hiyo wakati wa usiku. Katibu Mkuu wa NAMETWA na Mwakilishi wa TAWU Digital Taxi Bw Wycliffe Alutalala, alisema wenzake katika sekta hiyo wanahofia kufanya kazi majira hayo kwa kukosa wateja hata kwenye barabara.

“Usalama wetu ni muhimu sana. Tumezoea walevi ndio asilimia kubwa ya wateja wetu lakini sasa hivi ukipokea ombi a mteja kutaka umpeleke eneo jingine, unakuwa na wasiwasi kuhusu usalama kwani wakora pia wanamwagika mitaani usiku,” akasema Bw Alutalala.

KKatibu Mkuu wa NAMETWA na Mwakilishi wa TAWU Digital Taxi Bw Wycliffe Alutalala akiwa kwenye mahojiano na Taifa Jumapili. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Unajua ukipata mteja ambaye ni mlevi unakuwa hauna wasiwasi lakini ukipata mteja ambaye anataka umpeleke mitaa duni na si mlevi, unapaingiwa na wasiwasi. Hii ni kwa sababu labda anapotaka uende ni mbali na hujui ana nia gani,” akaongezea.

Bw Alutalala, alisikitishwa na baadhi ya wateja ambao wakati mwingine hutafuta huduma zao, japo wana nia tofauti.

“Ombi langu kwa serikali ni kuwa ituhakikishie kuwa usalama upo. Hatukatai pombe haramu ni mbaya, lakini sisi tunayo magari ambayo tunafaa kulipia mikopo. Wengi wamekuwa wakifanya kazi hii usiku ambapo wateja huwa wengi. Hatujui tutalipa mikopo yenyewe vipi,” akatoa rai.

Ripoti ya Utafiti kutoka kampuni ya huduma za teksi ya Uber inaonyesha kuwa Kenya ina madereva zaidi ya 30,000 wanaotoa huduma za usafiri zinazotegemewa na zaidi ya wasafiri 2 milioni.