HabariSiasa

MSALITI AU MZALENDO: Jinsi kuwa Raila Odinga si kazi rahisi

September 24th, 2018 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MWELEKEO mpya wa kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga wa kuunga mkono maamuzi ya serikali ambayo hayazingatii maslahi ya mwananchi wa kawaida, umekanganya Wakenya kutoka mirengo yote ya kisiasa.

Mnamo Januari 30 mwaka huu, Bw Odinga alijilisha kiapo cha “rais wa wananchi” lakini mienendo yake inatilia shaka madai yake ya kuwa ni “Mtetezi wa Wanjiku”, ambaye sasa anamwona kama msaliti

Badala yake Bw Odinga ameonekana kuwa “Mtetezi wa Tabaka la Watawala” ambalo linamtaja kama mzalendo anayejali nchi yake.

Kulingana na wakereketwa ndani ya Serikali, Bw Odinga ni mzalendo ambaye alionyesha hilo alipokubali kufanya kazi na Rais Kenyatta, hatua ambayo ilileta

Lakini kwa wananchi Bw Odinga ni msaliti japo anawahakikishia wafuasi wake na Wakenya kwa jumla kwamba angali anawaelekeza Canaan (nchi ya ahadi).

Waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa akiwashangaza Wakenya kwa kuunga maamuzi ya serikali ambayo kabla ya muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akiyapinga vikali.

Wadadisi wanasema kile ambacho Bw Odinga anafanya ni kuunga Rais Kenyatta mkono na sio kuwakilisha maslahi ya wananchi.

Kwa Wakenya, Bw Odinga amebadilika na sasa anaonyesha sura yake kamili kwa kuunga sera za serikali zinazofanya maisha yao kuwa magumu zaidi.

Maamuzi na matamshi yake siku hizi ni tofauti na awali alipokuwa akijitokeza kukosoa serikali kwa hatua zozote za kuumiza mwananchi wa kawaida na kutetea haki zao.

Wafuasi wake ambao walikuwa wakiitikia mito yake ya kuandamana kupinga unyanyasaji, wakati huu wanashangaa alivyobadilika na kuwa mtetezi wa wanaokadamiza mwananchi kwa kuongeza gharama ya maisha.

Matamshi yake Jumamosi ya kuwapongeza wabunge wa chama chake walioshirikiana na wale wa Serikali kulazimisha mswada wa kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru, yamewaacha wengi wamechanganyikiwa.

Kulingana na Raila, Wakenya wanafaa kutozwa kodi hiyo ili shida zao ziweze kutatuliwa, lakini hajafafanua jinsi kuongeza mzigo wa ushuru kutakavyotatua shida za wananchi ambao wamesukumwa kwenye ukuta.

“Ninawahakikishia Wakenya kwamba nimejitolea kutafuta suluhu la kudumu kwa matatizo ya miaka mingi yanayowakumba,” alisema Bw Odinga kwenye taarifa ya kuwapongeza wabunge waliopitisha mswada wa ushuru mpya.

Serikali ilipopitisha sheria za usalama katika mazingira sawa na ya wiki jana ambayo yalikumbwa na fujo, kelele, mabavu na hila, Bw Odinga alikosoa hatua hiyo na kuongoza upinzani kuwasilisha kesi na sehemu kadhaa zikaondolewa kwa kukiuka Katiba.

Hatua yake ya kuunga mkono mapendekezo ya Rais ilijiri wiki moja baada ya kuwahakikishia Wakenya kwamba Rais angetia sahihi mswada wa fedha ambao wabunge walipendekeza utekelezaji wa ushuru wa mafuta uahirishwe.

Hakikisho hilo halikutimia na badala yake Rais alirudisha mswada huo bungeni akipendekeza hatua kali zaidi za utozaji kodi ambazo Bw Odinga mwenyewe ameunga mkono.

Kulingana na msemaji wake Dennis Onyango, Bw Odinga hajaacha jukumu lake la kuwa tetea Wakenya dhidi ya ukadamizaji wa serikali.

“Alichofanya ni kubadilisha mbinu. Aligundua kuwa mbegu ya matatizo ya nchi hii ilipandwa miaka mingi iliyopita na haiwezi kung’olewa kupitia mikutano ya wanahabari.

Kama ni kuandamana, tumeandamana, kama ni kukosoa, tumekosoa lakini hakuna kilichobadilika ndiposa aliamua kumuunga mkono Rais,” alisema Bw Onyango akiongea na Sunday Nation. Lakini mbunge mmoja wa ODM aliyeomba tusitaje jina lake ana maoni tofauti: “Kwa sasa kile Wakenya wanaona ni Raila Odinga halisi.

Kwamba anapowaita barabarani huwa ni kumsaidia kutimiza malengo yake. Wale waliokufa wakati wa maandamano ni shauri yao, inasikitisha.”

Mbunge huyo anasema wafuasi wa Raila waliokuwa na matumaini makubwa kwake wanahisi amewasaliti: “Kumbuka kwamba Raila aliamuru wabunge wa ODM kuunga mapendekezo ambayo anafahamu kwamba yanaumiza Mkenya wa kawaida, kama huo sio usaliti ni Canaan gani? alisema na kuongeza kuwa muafaka wake na Rais ulimfanya mateka hivi kwamba hawezi kukosoa serikali.

Tangu atangaze muafaka wake na Rais Kenyatta, Bw Odinga hajawahi kuikosoa chochote.

Amewahi kunukuliwa akisema hana haja ya kukosoa serikali kwa sababu siku hizi anawasiliana moja kwa moja na Rais Kenyatta.