HabariSiasa

MSAMAHA: Unafiki katika maombi

May 30th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wanapokutana Alhamisi kwa maombi ya kitaifa ya mwaka huu katika hoteli ya Safari Park, Nairobi, unafiki wao unajitokeza kutokana na kukosa kutimiza msamaha waliotangaza hadharani kwenye sala za 2018.

Kwenye maombi ya mwaka uliopita, Rais Uhuru Kenyatta aliongoza naibu wake William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wa Wiper kukumbatiana na kutangaza kusameheana.

Hatua hiyo ilileta matumaini makubwa kuwa hatimaye wangeshirikiana kuleta umoja wa kitaifa, kukomesha siasa za chuki, kupigana na ufisadi na kujenga taifa lenye ustawi.

Wakisimama mbele ya wageni walioalikwa na kutazamwa moja kwa moja na Wakenya kwenye televisheni, viongozi hao waliahidi kutuliza joto la kisiasa hadi 2022, kuunganisha Wakenya, kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi na kuhubiri umoja wa kitaifa.

Kilele cha maombi hayo kilikuwa ni vigogo hao kuombana msamaha hadharani na kukumbatiana kwa makosa waliyotendeana na kuwatendea Wakenya wakati wa chaguzi mbili za urais 2017 .

“Tulishiriki kampeni kali yenye ushindani, kuitana majina na kurushiana lawama za kila aina. Lakini hapa leo, mbele ya watu hawa na Wakenya kwa jumla, ninaomba msamaha bila masharti,” Rais Kenyatta alimwambia Bw Odinga

Naye Bw Odinga aliomba msamaha kwa niaba ya muungano wa NASA na tangu wakati huo wawili hao wanaonekana kudumisha ahadi yao.

“Kwa niaba yangu binafsi na chama chetu cha Jubilee, na kufuata nyayo za viongozi hawa wa kuigwa (Rais Kenyatta na Bw Odinga), ndugu yangu Stephen, ninakuomba msamaha,” Dkt Ruto naye alisema na kuwakumbatia Bw Musyoka na Bw Odinga.

Lakini mara baada ya kuteremka jukwaani, Dkt Ruto na Bw Odinga walisahau walikuwa wamesameheana na mara moja pamoja na wandani wao wakaendeleza malumbano ya kisiasa.

Tangu hapo wawili hao wamekuwa wakiongoza washirika wao kushambuliana vikali hasa kuhusu vita dhidi ya ufisadi na mageuzi ya kikatiba.

Tofauti zao zimezidi huku Dkt Ruto akimlaumu Bw Odinga kama tapeli wa kisiasa anayetaka kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma na kuvuruga chama cha Jubilee.

“Hatutakubali propaganda katika serikali. Waliungana nasi kubadilisha nchi lakini nia yao ni kuvunja chama cha Jubilee na serikali. Tunawaambia kwamba tunawatazama,” Bw Ruto amekuwa akidai.

Uhusiano wa Rais Kenyatta na naibu wake pia umekuwa baridi tangu mwafaka wa handisheki mwaka jana.

Bw Odinga na washirika wake naye hajaachwa nyuma kumshambulia Dkt Ruto na wamekuwa wakieneza kampeni ya kutaka kumwonyesha Naibu Rais kama anayetatiza vita dhidi ya ufisadi.

Kwenye maombi ya kitaifa ya 2018, ambapo waliombana msamaha, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa vita hivyo havilengi jamii moja, jambo ambalo Dkt Ruto na washirika wake wanasisitiza.

Uhasama wa kisiasa umezidi hivi kwamba wanasiasa wa upinzani wanaoshirikiana na Bw Ruto wamekuwa wakionywa na hata kutimuliwa katika vyama vyao.

Kulingana na Pasta Sam Mboto wa Great Mission Church, malumbano ya viongozi hawa yanaweza kuzua uhasama na chuki za kijamii nchini.

“Viongozi wanapaswa kuwa mfano mwema wa kuigwa na wanaoongoza. Wakitoa msamaha hewa, wafuasi wao watawaiga,” asema.