Habari

Msando atuzwa kimataifa kwa uadilifu wa uchaguzi wa 2017

February 4th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

TUZO ya heshima imetolewa kwa aliyekuwa Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), mwendazake Bw Chris Msando.

Tuzo hiyo ya uadilifu katika usimamizi wa uchaguzi ilipeanwa na shirika la International Centre for Parliamentary Studies, wakati wa kongamano la 17 la masuala ya usimamizi wa uchaguzi lililofanywa Ghana wiki iliyopita.

Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati pia alituzwa kwa usimamizi bora wa mizozo ya uchaguzi.

Bw Msando aliuawa kikatili jijini Nairobi kabla Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2017 na mwili wake ukapatikana mwituni ukiwa na majeraha mabaya ya kukatwakatwa na kunyongwa.

Aliyekuwa Kamishna wa IEBC, Bi Roselyn Akombe alisifu hatua ya kumtuza marehemu kwani itasaidia kuendeleza sifa alizoacha, na pia ni thibitisho la jinsi mtume huheshimiwa kila mahali isipokuwa anakotoka.

Chanzo halisi cha mauaji yake kimesalia kuwa kitendawili licha ya ahadi zilizotolewa na serikali kuwasaka na kuchukulia hatua wahusika.