Makala

Msanii aliyeimba kumsifu Ruto sasa ahofia maisha yake

Na MERCY KOSKEI August 9th, 2024 1 min read

MWANAMUME aliyetunga wimbo wa kumsifu Rais William Ruto na muungano Bw Gideon Kipkorir, 30, alitunga wimbo kwa jina “Kenya Kwanza” miaka miwili iliyopita akidhamiria kuonyesha kipaji chake na kupata riziki.

Msanii huyo kutoka Kaunti ya Nakuru aliyekuwa anaishi kama chokoraa hapo mbeleni, alitunga wimbo huo kusifu uongozi wa Rais Ruto, serikali yake na sera zake za maendeleo kuanzia mashinani.

Kibao hicho cha Kipkorir kilivuma mno na kupokelewa vyema na wafuasi wa Dkt Ruto likipata umaarufu miongoni mwa vijana.

Hata hivyo, kilichoanza kama ishara ya uzalendo kimegeuka mashaka na kumsababishia aibu na dhihaka mwanamuziki huyo, kufuatia maandamano ya kupinga serikali.

Huku maandamano ambayo yamegeuza mwelekeo wa kisiasa yakizidi kuchacha nchini, Kipkorir ameshambuliwa na vijana wanaohisi anamsifu Rais wakati huu mgumu kiuchumi.

Mwanamuziki huyo anaishi kwa hofu huku akizidi kushambuliwa na kutumiwa vitisho.

“Sikuwahi kufikiri kuwa muziki wangu uliokusudiwa kuonyesha kumuunga mkono (Ruto) ungetia maisha yangu hatarini. Ninaogopa hata kutoka nje kusaka vibarua kwa sababu kila mara ninapoendelea na shughuli zangu, huwa ninakabiliwa na watu wenye chuki,” Kipkorir alieleza Taifa Leo Jumatano.

Alisimulia visa ambapo alishambuliwa na makundi ya vijana waliomwitisha pesa au kumlazimisha kujiunga na maandamano ya kupinga serikali mwezi uliopita.

Visa hivyo vimemlazimu kuacha biashara yake ya bodaboda iliyokuwa ikimpa riziki.

Masaibu ya Kipkorir yalianza alipovamiwa na vijana wakati wa maandamano kabla ya kuvamiwa akielekea kazi ya ujenzi.