Chipukizi asimulia machafuko ya 2007 yalivyomchochea kujitosa kwa usanii wa injili

Chipukizi asimulia machafuko ya 2007 yalivyomchochea kujitosa kwa usanii wa injili

NA WANNIE  ONYANDO 

Wengi wanapitia changamoto nyingi maishani. Anayohitaji mtu ni maneno yatakayompa motisha na tumaini.

Kando na kuburudisha, nyimbo za injili zina umuhimu hasa kupitia ujumbe kutoka maandiko takatifu unaofariji na kumpa mtu matumaini anapokata tamaa.

Shida yanaweza kumfanya mtu akose amani moyoni na hata kuchukulia kuwa pengine amelaaniwa. Ila kupitia ujumbe wa nyimbo za injili, mtu kama huyo atapata faraja na imani yake kuwa thabiti.

Hayo ndiyo kauli ya kijana barobaro mkorino Paul Kimani almaarufu PK Hakeem, 22, anayeimba nyimbo za injili.

Kimani ambaye ni mzaliwa wa pili katika familia ya watu nane anasema kuwa japo alizaliwa Kericho, alilelewa katika mtaa wa London Hilton kaunti ya Nakuru kutokana na machafuko ya kisiasa wa mwaka wa 2007.

Kijana huyo anasema kuwa walilelewa katika shida hasa baada ya vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007.

“Tuliathiriwa sana na uchaguzi wa 2007 tukawa wakimbizi. Tulipelekwa katika mtaa wa London ambapo tumeishi tukitegemea usaidizi kutoka kwa serikali,” Kimani aliambia Taifa Leo.

Kimani anaeleza kuwa kupitia bidii ya wazazi wake, alipelekwa katika Shule ya Msingi ya Milimani na baadaye kuhamishwa katika shule ya kibinafsi ya Junior ambapo alifanya mtihani wake wa KCPE.

Baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi, alipelekwa katika Shule ya Upili ya Crater View ambapo alipasi mtihani wake wa KCSE.

“Kwa kuwa wazazi walikosa karo, sikujiunga na chuo jinsi ilivyotarajiwa bali nilikaa nyumbani mwaka mmoja na baadaye kujiunga na kikundi cha uigizaji cha Nakuru Players Theatre,” alisema Kimani.

Kama wazazi wengine, Kimani anaeleza kuwa wazazi wake walichukulia uimbanji kama talanta duni na ambayo haina faida. Anaeleza kuwa kila mtu kwao alimchukia kwa sababu ya uamuzi wake wa kuwa mwanamuziki.

“Hakuna mwanamuziki kwetu, kila mtu anachukia kuimba. Ndugu yangu mkubwa Mariko Njuguna ndiye aliyenipa mkono na kuniombea dua kila mara,” Kimani alikiri.

Mwaka wa 2019 alijiunga na Taasisi ya East Africa Institute of Certified Studies (EAISC) ambapo anasomea uwanahabari. Masomo yake yalikatizwa baada ya serikali kusimamisha masomo katika taasisi zote za kielimu kutokana na ugonjwa wa corona.

Kimani alieleza Taifa Leo sababu zake kuu za kuimba muziki za injili ni mateso waliyopitia kama familia baada ya vurugu za kisiasa wa 2007.

Aliutumia wimbo wake wa kwanza ‘Kumbuka 2007’ kueleza ghasia za kisiasa na jinsi walivyoathiriwa.Wimbo huo pia anautumia kuwahimiza watu waliopitia tatizo kama yake. Hadi sasa, kijana huyo anasema kuwa ameandika nyimbo zaidi ya 10 na kutoa nyimbo nne.

Wimbo wake wa ‘Mwabudu’ aliutoa mwaka wa 2020 katika studio ya EMB Records Nakuru. Nyimbo za ‘Ndani ya Yesu’ na ‘Kwa Yesu Niko Simple’ alizitoa mwaka huu wa 2021.

Anasema kuwa kupitia wimbo wake wa ‘Mwabudu’, aliweza kuteuliwa mshindi katika Great Rift Valley Gospel Music Awards 2020 katika kitengo cha msanii barobaro wa nyimbo za injili, jambo lililomtia moyo katika sekta ya muziki.

Kando na kuimba, kijana huyo anasema kuwa anatumia talanta yake ya uigizaji katika kujichumia hela.

Tangu ajiunge na Synet Theatre Production, wameweza kuigiza vitabu kama vile Kidagaa Kimemwozea, The River and the Source, Kigogo, Betrayal in the City, Caucasian Chalk Circle, Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine, Blossoms of The Savannah, Chozi la Heri na The Pearl katika shule mbalimbali za Sekondari.

“Pesa ninazopata kupitia uigizaji zinanisaidia sana katika kuendeleza talanta yangu ya kuimba. Nimetumia hela hizo kutoa nyimbo zangu zote,” Kimani aliambia Taifa Leo.

Wameweza kuigiza vitabu hivyo katika shule ya Sekondari ya Butere Girls, Friends School Kamusinga, St Agnes Nakuru, St Kizito miongoni mwa nyingine.

Waliweza pia kuigiza mchezo wa Luanda Magere mwaka wa 2020. Nyimbo zake zote amezipakia katika mtandao wa kijamii ya Twitter, Instagram, Facebook, Audio max, Spotify na YouTube na anatumia jina la pkhakeem.

Anawashukuru wafuasi wake na kuwaamba waendelee kusimama naye kwa mali na ghali.

You can share this post!

‘Lockdown’ ya Aprili 2021 ilivyoyumbisha biashara yake...

Oimeke wa ODM aibuka mshindi wa kiti cha ubunge Bonchari