Msanii ‘Lonely Man’ awaumbua mabinti wapenda pochi

Msanii ‘Lonely Man’ awaumbua mabinti wapenda pochi

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

KUTOKANA na kuonekana na kupata sifa kutoka kwa wazazi na waalimu alipokuwa akiimba nyakati za sherehe za shule, ndiko kulikomuongoza kwenye njia ya kuwa mwanamuziki wa kutambulika.

Ibrahim Kazungu almaarufu Lonely Man alianza kupenda kuimba tangu alipokuwa shule ya msingi ambako alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiwatumbuiza wazazi kila kulipotokea sherehe za shuleni.

Lonely Man ameanza safari yake ya kuwa mwanamuziki mwenye kutambulika katika Kaunti ya Mombasa huku akisambaza umaarufu wake kwengineko jimbo la Pwani.

Lonely Man anasema waalimu wa shule alizosoma ya msingi ya Jamvi Primary na ya upili ya Soan Education Centre ndio waliompa motisha wa kuendeleza kipaji chake ambacho kilitambulika kwenye hizo.

“Nilikuwa nikisisitizwa na waalimu wakati nilipokuwa nashiriki kwenye Music Festival kuchukulia muziki kuwa muhimu nilipofika kidato cha tatu ndipo nilifanikiwa kutoa kibao changu cha kwanza,” akasema msanii huyo.

Kibao chake cha kwanza kilikuwa kile cha ‘Hela kitu’ ambacho kilikuwa cha audio ambacho kiliitikiwa vizuri hadi akamvutia DJ Lenium kumualika kwenye shoo yake katika baa ya Valencia iliyoko katikati ya mji wa Mombasa.’

“Nimeimba kibao hicho kwa sababu ya kuwalaumu wasichana kwa tabia ya kupenda pochi ndipo wakubali pendo. Niliimba ili wasichana wenye busara wasifuate mwendo huo,” akasema.

Lonely Man hakutosheka na wimbo huo mmoja kwani kabla ya kumaliza masomo yake ya kidato cha nne, aliweza kuzindua nyimbo yake ya pili ya ‘Safari’ akimaanisha kuwa ameanza safari yake ya kutamba katika muziki.

Katika nyimbo hiyo, msanii huyo aliwashirikisha wenzake wawili, Naxynovenomz na Hassan, wimbo ambao haukuitikiwa sana. “Sikuvunjika nguvu kwani nilitambua kuwa mafanikio hayapatikani kirahisi kwani lazima upande na kushuka mabonde.

Kabla ya kumaliza masomo yake, alishirikiana na wenzake kuunda kikundi cha wasanii kwa jina la Voltre Gang ambalo liko hadi wakati huu ingawa mara nyingi huwa anaimba nyimbo zake mwenyewe.

Baada ya kumaliza shule na japokuwa kulikuwa na janga la corona, Lonely Man aliweza kumudu kutoa kibao chake cha tatu cha ‘Down low’ ambacho amekitoa kwa minajili ya kuwafanya mashabiki wake wapate kunengua na kufurahikia mtindo mpya wa gengetoni. PICHA/ ABDULRAHMAN SHERIFF

 

Lonely Man ana nia ya kufanya kazi na wasanii wenye majina makubwa kwa sababu hapo ndipo atakapotambulika na kuwa maarufu. Alitoa mfano wa msanii Zuchu wa huko Bongo akisema mara alipoimba na Diamond, alipanda ngazi kiasi cha kuwa maarufu kote duniani.

Anasema anamshabikia na kufurahikia nyimbo anazoimba Mr Blue wa huko Tanzania kwa sababu ya mtindo wake wa kuimba nyimbo za Hip Hop. “Nina hamu kubwa ya kukutana na Mr Blue na nitafurahikia nikipata fursa ya kuimba naye,” akasema.

Hapo kwao Mombasa, Lonely Man anasema anapendelea nyimbo za Kalamoto ambaye ni mmojawa wasanii marufu wa jimbo la Pwani. Anasema anamnyemelea kufanya kolabo naye kabla yam waka huu kumalizika.

Mwanamuziki huyo anasema yuko njiani kuzindua nyimbo zake sita kabla ya mwisho wa mwaka huu. Nyimbo ambazo anasubiri kuzizindua ni ‘Baba’, ‘Kupambana’, ‘Tinsgisha’, ‘Scamaree’, ‘Haga’ na ‘Wivu’.

Katika nyimbo zake, anatumia mitindo ya Bongo Fleva na Gengetone, mtindo mpya ambao unaendelea kutamba hasa jijini Nairobi. “Nina imani nitafanikiwa kuinua kipaji cha uimbaji wangu na kuweza kuwa mmoja wa wanamuziki mashuhuri nchini Kenya.

Nia yake kubwa ni kutaka kufanikiwa na kuwa mwenye kipato kikubwa ili pate kuwasaidia wanamuziki chipukizi ambao wamekuwa wanapata shida hata kutoa nyimbo zao kutokana na ukosefu wa fedha.

Aliwalaumu viongozi wa Pwani kwa kukosa kuwasaidia wasanii wanaoinukia bali wanapoteza pesa nyingi kuagiza waimbaji kutoka nje ya nchi na kuwalipa malukuki ya fedha.

You can share this post!

Kimani kuidhinishwa rasmi naibu kocha Bandari

Kositany asema ataishtaki Jubilee kwa kumtimua