Habari za Kaunti

Msanii Mbosso alivyotumbuiza wakazi Kilifi kukaribisha 2024

January 1st, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

MSANII wa Bongo kutoka Tanzania, Mbwana Yusuf maarufu kama Mbosso Jumapili usiku, Desemba 31, 2023 aligeuza ufuo wa bahari wa Old Ferry Creek, Kilifi uga wa makaribisho ya mwaka mpya 2024.

Mamia ya wakazi na mashabiki wake walijitokeza kutangamana naye, kupitia matumbuizo yake ya ana kwa ana.

Katika harakati za kuukaribisha Mwaka Mpya, wakazi wa Malindi pia waliweza kufurahia burudani baada ya serikali ya Kaunti ya Kilifi kuandaa tamasha lake lililofanyika katika ukumbi wa bustani ya Buntwani Waterfront Park.

Ambapo wasanii chipukizi kutoka eneo hilo walipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao akiwemo Jumaa Bakari almaaruf Raa Touch, Pokomo Princess, Yemi Geng na kisha baadaye msanii tajika kutoka Pwani Yusuf Kombo almaaruf Susumila aliweza kunogesha tamasha hilo.

Msanii tajika kutoka Kaunti ya Kilifi Peter Siku almaaruf P-Day alipata nafasi ya kuonyesha weledi wake wa kuimba baada ya kupanda steji moja na Susumila na kuimba wimbo wake aliomshirikisha Susumila.

Maelefu na mamilioni ya Wakenya walikongamana katika maeneo ya kuabudu, na wengine kwenye baa na maeneo ya burudani kukaribisha 2024.

Rais William Ruto, alihutubia taifa akiainisha miradi ya maendeleo aliyofanya 2023 na matarajio ya serikali yake – Kenya Kwanza 2024.