Bambika

Msanii Nyashinski ateswa na kesi mahakamani

February 18th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

KESI ya rapa Nyashinski imepigwa kalenda hadi Machi 13, 2024, ambapo anashtakiwa na produsa raia wa Nigeria kwa kutomshirikisha kwenye dili tamu ya ubalozi anayoamini msanii huyo alilambishwa kiasi kisichopungua Sh12 milioni.

Sam Eli alienda mahakamani mwaka 2023 na kumshtaki Nyashinski kwa madai ya uvunjaji wa hakimiliki ya kwake.

Eli ndiye produsa aliyeandaa ngoma hiti ya yake Nyashinski, Wach Wach.

Ngoma hiyo ilitumika sana kuitangaza simu ya Tecno Camon 20 ikiwa ni baada ya Nyashinski kusaini dili ya ubalozi na kampuni hiyo ya kutengeneza simu ya China.

Wach Wach ilikuwa miongoni mwa nyimbo sita alizomwandalia Nyashinski.

Eli aliieleza mahakama kwamba jitihada zake za kusaka mgao wa dili hiyo kutoka kwa Nyashinski ziliambuliwa patupu kwani jamaa ameishi kumkaushia.

Alipotishia kumshtaki, Eli anadai Nyashinki alimpa ofa ya Sh50,000 ili adondoshe kesi hiyo na maisha yaendelee.

Kesi hiyo ilisikilizwa mara ya kwanza juzi kati ambapo hakimu alimwamrisha Nyashinski kuwasilisha mkataba aliosaini na Tecno.

Aidha Nyashinski aliamrishwa kuwasilisha ripoti zote za mapato ya ngoma hiyo alizopokea kupitia strimu.

Kwa maana hiyo, jaji kampa Nyashinski muda wa mwezi mmoja kufanya hivyo na sasa kesi itasikilizwa tena Machi 13, 2024.