Msanii wa nyimbo za injili anayesaidia watoto mitaani

Msanii wa nyimbo za injili anayesaidia watoto mitaani

NA PETER CHANGTOEK

YEYE ni msanii wa nyimbo za injili ambaye amejitolea mno kulitukuza neno la Mungu kupitia kwa nyimbo zake.

Aidha, amekuwa akiwasaidia watoto wanaorandaranda mitaani kwa kutumia hela zake.

Si mwengine, bali ni Christine Otieno, ambaye amejulikana mno kwa wimbo wake Yesu Nyale, mbali na kujulikana kwa nyimbo zake nyinginezo.

Hata hivyo, anasema kuwa, maisha yake ya hapo awali hayakuwa rahisi. alizipitia changamoto kadhaa, ndiposa akawa na utu wa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.

“Nilipitia shida nyingi sana; kwa hivyo, nikiona watu wakiteseka, huwahurumia sana. Lazima niwasaidie,” asema.

Christine, aliyezaliwa katika eneobunge la Rarieda, anasimulia jinsi maisha yake yalivyokuwa, kabla hajaja Nairobi, ambako nyota yake ilianza kung’aa.

“Kwa kweli nilipitia changamoto nyingi, lakini namshukuru Mungu kwa yale ambayo amenitendea,” asema msanii huyo.

“Mama yangu aliondoka nyumbani wakati babangu alipomwoa mke wa pili. Nilibaki na ndugu zangu wawili wakubwa,” asema, akiongeza kuwa, ilibidi nyanya yake amtunze.

Anasema kuwa, alipokuwa na umri wa miaka minane, akiwa katika Darasa la 4, alishurutika kuuza kuni na samaki aina ya dagaa, katika soko la Oyude, katika kituo cha biashara cha Akala.

“Nilikuwa nikilazimika kuondoka shuleni kabla ya saa tisa, ili nibebe kuni na dagaa kuuza ili tupate chakula,” aeleza, akiongeza kuwa, mama yake alirudi nyumbani alipokuwa katika Darasa la 6.

Baada ya kufanya mtihani wa KCPE, alifuzu vyema na kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyakongo, kule Uyoma.

Hata hivyo, alilazimika kuacha masomo yake akiwa katika Kidato cha 2, baada ya baba yake kudinda kuendelea kumlipia karo.

“Pindi tu nilipoingia katika Kidato cha Pili, babangu alikataa kunilipia karo, akidai kuwa wasichana hawafai kusomeshwa, ila wavulana tu ndio wanaofaa,” asimulia.

Alishurutika kukatiza masomo yake ghafla bin vuu. Maadamu nyanya yake alikuwa akimpenda mno, alimkabidhi Sh10, ili azitumie kuanzisha biashara ya kununua na kuuza dagaa.

Alianza kwa kununua kilo mbili, pasi na kujua kwamba, biashara hiyo ingekuja kumfaa kwa hali na mali. Biashara hiyo ilinoga sana, kiasi kwamba aliweza kupata Sh23,000, alizozitumia kuirekodi albamu yake ya kwanza.

“Nilikuja Nairobi na kutumia kiasi fulani cha pesa hizo kulipia kozi ya ushonaji katika soko la Kariobangi. Punde tu nilipomaliza kozi hiyo, nikapata kazi, ambapo nilikuwa nilipwa Sh2,700 kwa mwezi,” afichua msanii huyo.

Baada ya kuirekodi albamu yake ya kwanza mwaka 2007, mambo yake yakaanza kunyooka, na anasema anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kufika alipo kwa sasa.

Msanii wa nyimbo za injili, Christine Otieno. PICHA | PETER CHANGTOEK

Msanii huyo, ambaye kwa sasa ana shahada kwa maduala ya biashara, ana albamu nyingi alizozirekodi. Ana nyimbo nyingine kama vile; Rafiki Mwema, Haijalishi Wasema Nini, Warruok, Nyasach Israel, Honde, Agombo Ngima, Musalaba, Yesu Luongoi, Ma E Ndalo, Wokovu Uko Wapi, Ng’wono Mar Nyasaye, Ngimana Nie Lweti, Yesu Emanyalo, Gigo Mitimo, Ofunguu, Nitabaki Nawe, Warruok, Nyasach Israel, Honde, Agombo Ngima, Musalaba, Yesu Luongoi, Ma E Ndalo, Wokovu Uko Wapi, Ng’wono Mar Nyasaye, Ngimana Nie Lweti, Yesu Emanyalo, Gigo Mitimo, Ofunguu, na Nitabaki Nawe.

Pia, ana nyingine kama vile; Yesu Oromo Pako, Okumba Miya Ler Moromo, Sibuor, Ingeya Kod Nyinga, Mtetezi, Simba, Shangilia Yesu Anaweza, Oloyo Lweny, Wach Achiel, Onyoso Wuon Moo, Yesu Wololo, Yesu Nyale, Wololo, Olemo, Tie Mar Yesu, miongoni mwa nyinginezo.

  • Tags

You can share this post!

IEBC yakosa kutaja vituo visivyo na mfumo wa kisasa kutuma...

Uhuru ateua majaji saba wapya katika mahakama ya rufaa

T L