Msasa wa mawaziri wa Sakaja kuendelea

Msasa wa mawaziri wa Sakaja kuendelea

NA RICHARD MUNGUTI

BUNGE la kaunti ya Nairobi limekubaliwa kuendelea kuwapiga msasa watu 10 waliopendekezwa na Gavana Johnson Sakaja kuwa mawawiri katika serikali ya kaunti ya Nairobi.

Mahakama ya Kuamua Mizozo kati ya Waajiri na Wafanyakazi (ELRC) ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na vuguvugu la mawakili la kutetea haki za jamii ya Wanubi lililodai Bw Sakaja hakumteua Mwislamu katika baraza lake la mawaziri.

Akitoa uamuzi Jaji Anne Mwaure alisema kesi hiyo iliwasilishwa kortini haraka kabla ya bunge la kaunti ya Nairobi kukamilisha zoezi la kuwapiga msasa watu 10 aliowapendekeza Bw Sakaja.

Mahakama iliamuru zoezi hilo la kuwateua mawaziri hao lirejelewe.

Walalamishi walidai Bw Sakaja hakuzingatia makundi yote katika jamii alipowapendekeza watu watakaotwaa nyadhifa za mawaziri.

Aliowapendekeza Bw Sakaja kutwaa nyadhifa mbali mbali ni pamoja na Charles Kerich, Brian Mulama, Patrick Mbogo, Stephen Mwangi, Ibrahim Auma, Rosemary Kariuki, Maureen Njeri, Anastacia Mutethia na Susan Silantoi.

Katika orodha hiyo ni pamoja na Michael Gumo, mwanawe aliyekuwa Mbunge wa Westlands Fred Gumo.

Bw Sakaja amemdumisha Bw Musumba kuwa katibu wa Kaunti.

Msimamizi wa wafanyakazi ni David Njoroge, Lawrence Wambua ni mshauri mkuu wa Sakaja katika masuala ya uchumi na biashara.

Wakili Elias Mutuma ni mshauri wake wa masuala ya kisheria, naye Samora Otieno (mshauri wa masuala ya afya), William Ndung’u ‘Fazul’ (mshauri wa kisiasa) na Washington Yotto Ochieng ni mshauri wake wa masuala ya uchukuzi.

Jaji Mwaure alikubaliana na wakili Duncan Okatch kwamba mawaziri hao hawakuwa wameidhinishwa na kwamba kesi hiyo iliharakishwa.

“Watu hawa wamependekezwa tu na kuidhinishwa kwao kutahalalisha nyadhifa hizo,” alisema Jaji Mwaure.

Mahakama ilielezwa kesi hiyo ilikuwa inaleta mkinzano kati na kuzua tofauti za kidini.

Bw Okatch alisema Gavana Sakaja hakukosea kuwateua watu hao 10 ikitiliwa maanani Kenya kuna makabila 45 na dini zaidi ya tano ikiwa ni pamoja na ile ya makafiri.

Jaji Mwaure alielezwa Sakaja angaliwateua watu 45 kutoka kila kabila na dini.

Mahakama ilisitisha kupigwa msasa kwa watu 10 Novemba 8, 2022.

You can share this post!

Afisa wa KDF akiri kupokea hongo ya Sh2.4 milioni kusaidia...

Kampuni ya Thiwasco yashirikiana na shirika moja la Denmark

T L