Habari Mseto

Mshairi atishia kuishtaki shule kwa kuiba ubunifu wake

August 16th, 2018 2 min read

Na NICHOLAS KOMU

VIONGOZI wa Mashindano ya Tamasha za muziki nchini wamekanusha vikali madai ya mshairi mmoja kwamba shairi lake liliwasilishwa katika tamasha hizo zinazoendelea mjini Nyeri.

Mwenyekiti wa tamasha hizo, Peter Wanjohi Jumatano alikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mshairi huyo hakuwasilisha ushahidi tosha kuthibitisha madai yake.

“Hakukuwa na ushahidi kwamba kazi yake ilikuwa imeigwa na kuwasilishwa. Shule husika ilikuwa huru kuchagua shairi lolote lililokuwa katika kategoria ya mashairi yaliyotungwa na mtunzi waliomchagua. Kamati haiwezi kuwajibikia hilo,” akasema.

Mshairi huyo kwa jina Waruguru wa Kiai anashutumu Shule ya Wasichana ya Sacred Hearts Mirithu kwa kuhariri shairi lake na kuliwasilisha Jumatano katika tamasha hizo.

Kulingana na sheria, shule zinaweza kuigiza au kuwasilisha shairi la watunzi mbalimbali mradi tu wamtambue mtunzi wa shairi husika.

Hata hivyo, Bi Kiai ametishia kuwashtaki mahakamani waandalizi wa tamasha hizo na shule yenyewe kwa kosa la kuiga kazi yake na kuitumia katika mashindano hayo.

Wasichana kutoka shule hiyo ya eneo la Kati waliwasilisha shairi lenye mada Take me to Nyeri (Nipeleke Nyeri) ambalo Bi Waruguru anadai mada yake halisi ilikuwa All I want for valentines.

Ingawa shule ilimtambua katika shairi hilo kama mtunzi, amelalamika kwamba kazi yake ilinakiliwa upya na kufanyiwa marekebisho machache, jambo analosisitiza ni kuigwa kwa kazi yake ya maandishi (Plagiarism).

“Ingawa walinitambua katika wasilisho lao, walibadilisha shairi langu, jambo ambalo haliruhusiwi kisheria.

Wangewasilisha shairi hilo jinsi lilivyoandikwa, jinsi inavyotakikana kisheria,” akasisitiza Bi Waruguru.

Vile vile Bw Wanjohi alifichua kuwa kamati yake haiwezi kuchukulia shule husika hatua za kinidhamu kwa kuwa mlalamishi tayari amekumbatia hatua za kisheria kutatua malalamishi yake.

“Mikono yangu imefungwa kwa sababu alishachagua utatuzi unaohusisha mahakama. Sasa atalazimika kukabiliana na mawakili wa wizara ya elimu,” akaongeza.

Wakati uo huo, kamati hiyo imetetea shule husika na kusema kwamba ilikuwa huru kuteua shairi hilo na kulibadilisha ili liweze kuoana na umri wa wanafunzi walioliwasilisha.

Pia, kamati ilitetea shule na kusema walitumia shairi hilo kwa masuala ya elimu wala sio kwa faida za kibiashara.

Aidha ilifichuka kwamba mtunzi huyo awali alishauriana na maafisa wa kamati na kufikia uamuzi wa shule hiyo kuruhusiwa kuwasilisha shairi lake ingawa mara ya kwanza aliwataka wasichana hao wasiruhusiwe kuliwasilisha.

“Niliamua kuwaacha wawasilishe kwasababu walikuwa wameshiriki mazoezi kabambe na kufuzu kutoka kiwango cha wadi hadi cha kitaifa. Hata hivyo nitafuatilia swala hili na maafisa hao pamoja na shule,” akasema Bi Waruguru.

Ingawa hivyo, shairi hilo liliorodheshwa katika nafasi ya sita katika kategoria ambayo mashairi ya shule za Moi Girls Eldoret, Ringa Boys na St. Mary Girls waliibuka wa kwanza, wa pili na watatu mtawalia.