Makala

MSHAIRI WETU: Bernard Mwandikwa almaarufu 'Mshairi wa Riaka'

September 11th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FANI ya ushairi ni kiungo muhimu katika jamii japo imekosa mapokeo mema katika kizazi cha Karne ya 21.

Isitoshe, wengi wamezembea katika kusoma na kung’amua maana fiche katika tungo za ushairi.

Mbali na kuelimisha, kuburudisha, kusifu, kukosoa ama kukashifu tabia fulani za binadamu, ushairi pia unatumiwa kama dira ya kutoa mwelekeo kwa jamii.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa katika Kata Ndogo ya Katumbi, Tarafa ya Masyungwa, Wilaya ya Tseikuru, Kaunti ya Kitui. Nimelelewa katika mandhari mbalimbali nchini Kenya, hali ambayo imenipa mtazamo mpana wa maisha, hususan nikiwa mshairi. Ijapokuwa nimesomea Uhandisi chuoni, ninapenda sana Ushairi wa Kiswahili.

Ulisomea wapi?

Katika shule mbalimbali za msingi na za upili. Shule za msingi ni: St Patrick Gilgil, St Andrews Malindi, Kakauni katika eneo la Tseikuru na Tala Township. Shule za upili ni: Kathiani Boys na AIC Kyome Boys.

Baada ya kufaulu katika mtihani wa KCSE, nilijiunga na Technical University of Kenya (TUK) kusomea Shahada ya Uhandisi (Electrical Engineering).

Nani na nini kilikuchochea kuupenda ushairi?

Utunzi wangu wa mashairi ulitokana na msukumo wa hali ya kimaisha baada ya kuishi maisha ya kuguragura kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hali hii ya kutembea kwingi, nilipata mtazamo mpana kuhusu hali ya maisha miongoni mwa jamii mbalimbali.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Nikiwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza shuleni Kathiani High. Lilikuwa shairi la kuisifu shule yangu.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Hali za kawaida katika maisha ya wanajamii wazawa wa Kiafrika na mabadiliko ya mitindo ya kufanywa kwa takriban kila kitu katika Karne ya 21.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Ninapoona matukio katika jamii, ya kupendeza na yasiyopendeza, huwa yananipa picha halisi ninazotumia kujengea dhamira za mashairi yangu.

Hukuchukua muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Iwapo nina mtiririko wa mawazo, shairi moja linaweza kuchukua takriban saa moja au mbili. Pia yapo mashairi yanayohitaji muda mrefu wa hata juma moja na zaidi ili kuyazamia kwa kina.

Mbona mashairi ya arudhi?

Uhodari wa mshairi hutambulika pale anapotumia maneno machache, kwa kuzingatia arudhi, ujenzi wa hisia, matumizi ya nahau na mbinu za kishairi bila ya kupoteza lengo katika ujumbe anaouwasilisha.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Nimekuwa nikichangia mijadala katika majukwaa mengi ya ushairi nchini Tanzania japo nimejifunza lahaja za Kimvita na Vumba. Tayari nimeandika kitabu changu kiitwacho ‘Riaka La Shairi’ ambacho natumai kitaboresha viwango vya usomaji na ufundishaji wa Ushairi wa Kiswahili.

Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na ushairi wako?

Nilituzwa cheti cha sifa njema kwa ubora wa uandishi wangu nikiwa mwanafunzi shuleni Kathiani Boys.

Mbali na kushiriki mashindano mbalimbali ya utunzi wa mashairi nikiwa Kyome Boys, ushairi ulinifanya kuwa Mwenyekiti wa Kundi la Wahariri wa Jarida la ‘Jitegemee’ shuleni Kathiani Boys.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Nadhamiria kutunga zaidi (mashairi na vitabu) na kusomea ushairi hadi kiwango cha Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Ninafanya kazi za uhandisi wa umeme, zaraa mamboleo na uandishi wa mada za kielimu na burudani za Karne ya 21.

Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako katika taaluma ya ushairi?

Chipukizi wasikate tamaa hata wakikosa mapokeo makubwa na mazuri katika kazi zao. Waliotutangulia katika fani wana jukumu zito na muhimu la kukuza vipaji vinavyochipuka, kuvinyunyizia maji na kuhakikisha vinanawiri kwa kuwaelekeza washairi chipukizi ipasavyo.