Makala

MSHAIRI WETU: Boaz Aseli 'Ustadh Kipepeo'

March 20th, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

WATU wengi hukata tamaa maishani kwa kuambiwa kuwa hawawezi kitu.

Katika maisha, twafaa kuwa na subira ambayo siku zote huwa ndio ufunguo wa milango ya heri.

Licha ya kudunishwa kwa maneno ya kutamausha nyakati fulani, mshairi chipukizi anastahili aendelee kujaribu tu hadi agundue jinsi ya kukabili baadhi ya changamoto za aina hii. Kujaribu ndiko kujua haswa!

Huu ndio ushauri wa mshairi Boaz Aseli ‘Ustadh Kipepeo’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa katika eneo la Lugari, Kaunti ya Kakamega na kulelewa mjini Kitale.

Mimi ni mtoto wa pili wa kipenzi mamangu Bi Brigid.

Uraibu wangu ni kusoma vitabu vya fasihi mathalan riwaya na diwani. Kwa sasa nasoma kitabu ‘Sitaki Simu’ chake Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya Greenfields, Kitale kisha nikajiunga na Shule ya Upili ya Kisii. Ila kwa sababu ya uchechefu wa hela za karo, ilinilazimu nimalizie masomo yangu ya sekondari katika Shule ya Upili ya Weaver Bird, Kitale. Nilifaulu vyema katika mtihani wa kitaifa wa KCSE na kujiunga na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Kakamega ambapo kwa sasa ninasomea kozi ya Ualimu katika masomo ya Hisabati na Biashara.

Nani au nini kilikuchochea kuupenda ushairi?

Tangu nikiwa mtoto, nilikuwa nikiwasikia watoto wenzangu wakighani mashairi redioni na kuvutiwa sana na upekee wa viwango vyao. Baadaye, nilianza kufuatilia vipindi vya Kiswahili kila Jumamosi huku hamasa zaidi ikichangiwa na weledi wa Nuhu Zubeir Bakari (Al Ustadh Pasua) enzi hizo akiwa QFM na QTV.

Nuhu ndiye aliyechochea kipaji changu cha utunzi. Natumia fursa hii kumwambia asante sana. Mbali na hilo, swahiba wangu Shuara Maxywelli amenimotisha mno.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Mnamo 2012 nikiwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza. Lilikuwa spesheli kwa dadangu Linda Elizabeth anayesoma kwa sasa katika Shule ya Msingi ya Sirende. Nilipania kumnasihi atie bidii masomoni.

Mashairi yako huegemea mada zipi?

Masuala ya huba na ndoa. Huwa nawaonya, kuwakosoa, kuwaelekeza na kuwaburudisha wasomaji kupitia mashairi yenye kujadili mada hizo. Aidha, mara kwa mara mimi hurejelea matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Nini hukuongoza kuteua mada hizi?

Huwa ni mambo ambayo yamenitendekea au niliyoona yakimtendekea mtu fulani katika jamii. Wakati mwingine mada hizi hutokana na habari runingani au redioni. Pia huwa napendekezewa mada na wandani wangu niwatungie mashairi.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Hunichukua takriban dakika 40 kutunga shairi la tarbia lenye beti saba hivi. Aidha, muda wa kutunga hutegemea sana maudhui ya shairi husika, bahari ya shairi, utulivu wa akili na vina nitakavyoteua. Baadhi ya maudhui huwa vigumu kutungia ilhali mengine ni mepesi. Kwa kutegemea upana au ufinyu wa uelewa wa msamiati, baadhi ya vina huwa ama rahisi au vigumu kuvipata.

Mbona mashairi ya arudhi?

Kwa sababu yanaweza kuimbika kwa mahadhi tofauti tofauti ya kuvutia. Utamu wa shairi ni kusikia mapigo ya sauti zenye urari linapoghaniwa aisee!

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Yasikitisha kwamba hakuna la mno kufikia sasa licha ya kujibidiisha katika utunzi.

Hata hivyo, naamini Jalali mwenye kujali atanijalia nyota yangu ing’ae hata zaidi katika siku za halafu, nije kuwa malenga maarufu wa kula na kushiba sifa. Kwa sasa ningali kiwavi anayekua na majaliwa nitakuwa kipepeo.

Nipepee kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo mbalimbali za haiba kubwa katika ulingo wa ushairi.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusu ushairi?

Tayari kuna mswada wa diwani ambao tumeandaa na upo katika matbaa. Unatushirikisha Wakenya wawili na Watanzania wawili. Mbali na kuandaa diwani nyingine kwa ushirikiano na wenzagu, napania kufyatua diwani yangu binafsi mwakani.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi hucheza kandanda. Nimekuwa golikipa stadi kuanzia shule ya msingi, ya upili hadi chuoni. Ningependa siku moja nivae glavu za Sofapaka.

Unawashauri nini washairi chipukizi na watangulizi wako katika taaluma ya ushairi?

Chipukizi wasife moyo. Wao ni kama maua ambayo yanahesabu siku kabla ya kuchanua na kuvutia vipepeo, nyuki na ndege. Washairi wa zamani wazidi kutuelekeza bila inda wala hiana.