Makala

MSHAIRI WETU: Dunneta Samama almaarufu ‘Malenga wa Mashinani’

September 4th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MASHAIRI yanaweza kutumiwa kuburudisha, kuelimisha, kuonya na hata kuipa jamii mwelekeo.

Mashairi pia hutumiwa kuwasilisha hoja fulani kwa jamii haswa kuhusu masuala yanayoibuka katika maisha ya kila siku.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Mimi ni kitindamimba katika familia ya Bw Paul Otiende na Bi Benta Otiende. Nilizaliwa katika Kaunti ya Siaya ingawa kwa sasa nalisukuma gurudumu la maisha katika eneo la Awendo, Kaunti ya Migori. Mungu amenijalia mtoto mmoja wa kiume, Paul Romey Jnr. Mimi ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Msingi ya Obama, Awendo. Pia ni mpenzi wa mpira wa kabumbu. Mbali na kutunga mashairi kwa Kiswahili na lugha yangu ya kwanza (Kiluo), napenda sana kuimba, kusakata densi, kusikiliza muziki na kuchekesha watu.

Ulisomea wapi?

Nilianzia masomo katika chekechea ya Railways jijini Mombasa kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Makande, Mombasa nilikofanyia mtihani wa KCPE.

Nilifaulu vyema na kupata nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Augustine Nyamoye, Siaya. Baadaye nilisomea ualimu katika Chuo cha Walimu cha St Paul’s Nyabururu, Kisii kisha kujiendeleza kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Kampala, Uganda.

Nimesomea pia katika Chuo cha KISE (Kenya Institute of Special Education), eneo la Kasarani, Nairobi. Huko ndiko nilikojifunza jinsi ya kuwasiliana kwa Lugha ya Ishara.

Nani na nini kilichokuchochea kuupenda ushairi?

Nilivutiwa na jinsi wakubwa wangu walivyokuwa wakiyakariri mashairi nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nilijipa moyo kuwa nami siku yangu ingefika ya kuyatunga na kuyakariri mashairi kama wao.

Pili, walimu wangu wa Kiswahili kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu walikuwa bora zaidi na ujuzi wao ulinichochea pakuwa kupenda ushairi.

Bi Akali na Lilian Otaba (Mungu amweke pema) walinitanguliza vyema zaidi katika Fasihi ya Kiswahili kabla ya Dkt Becky Wanjiku Omollo wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ghabba, Eldoret kuniamshia ari ya kuchangamkia utunzi wa mashairi ya kila sampuli.

Zaidi ya walimu wangu hawa, kunao washairi wengine ambao wamenihimiza mno. Hawa ni Victor Mulama,

Mstahiki Zack na George Ombetu. Wamenifunza kuwa ndugu ni kufaana, si kufanana.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Nilimtungia mwalimu wangu wa Kiswahili nikimshukuru kwa kunipa malezi bora ya kiakademia.

Mashairi yako huegemea zaidi mada gani?

Napenda kutunga mashairi ya mapenzi pamoja na yale yanayolenga kuwafunza watu jinsi ya kuishi vyema na wale ambao hawajabahatika katika jamii, hususan walemavu na maskini.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Matukio ya kila siku katika maisha pamoja na mapenzi yangu kwa walemavu na walalahoi. Hughasika sana ninaposikia au kushuhudia kundi hili la wanajamii likinyanyaswa.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Dakika 10 hivi ili kutunga shairi la beti nane. Utaalamu na ujuzi umekomaa!

Mbona mashairi ya arudhi?

Nayafurahia sana kwa sababu yanavutia na ni rahisi kuimbika. Hata hivyo, iwapo ujumbe utawafikia walengwa kupitia shairi huru, basi sina pingamizi.

Ushairi umekuvunia tija gani?

Nimefahamu idadi kubwa ya watu maarufu. Nimepata fursa nyingi za kughani na kukariri mashairi yangu katika hafla na mikutano ya kila aina. Nimepata tuzo anuwai na vyeti vingi.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Napanga kuchapisha kitabu cha ushairi. Pia napania kurekodi mashairi yangu ili yawafikie wasioweza kuyasoma magazetini na vitabuni. Nalenga pia kuchochea wengine waanze kuipenda sanaa hii.

Mbali na kutunga na (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi ni mzazi na mwalimu wa shule ya msingi.

Unawashauri nini washairi chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Chipukizi wajue kuwa bidii hulipa na mtafutaji hachoki. Wasichoke kutafuta hadi watakapopata. Washairi wa zamani waongoze chipukizi ipasavyo.