Makala

MSHAIRI WETU: Emmanuel Viambaka almaarufu Malenga Mcha Mola

September 25th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KAZI yoyote ya fasihi, haswa ushairi, huangazia maisha halisi ya binadamu kwa njia mbalimbali.

Masuala yote yanayobainisha taratibu za maisha ya binadamu yana uwezo wa kufichwa katika lugha ya kishairi na mtunzi akaimulika jamii pana kimtindo.

Haya ni maoni ya mshairi Emmanuel Viambaka almaarufu ‘Malenga Mcha Mola’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa kijijini Kivaywa, eneo la Matete katika Kaunti ya Kakamega. Nilisomea katika shule za msingi za Kivaywa na Shikusa katika Kaunti ya Kakamega kabla ya kujiunga na Tomena, Pokot Magharibi. Nilijiunga baadaye na Shule ya Upili ya Wavulana ya Ingotse, Kakamega kisha Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro, Kakamega. Kwa sasa nasomea shahada ya uzamili chuoni humo.

Nani na nini kilichokuchochea kuupenda ushairi?

Vipindi vya Kiswahili Redioni – Nuru ya Lugha (Radio Maisha) na Ramani ya Kiswahili (KBC), gazeti hili la Taifa Leo kupitia ukumbi wa mashairi, walimu wangu wakiwemo Jeff Mandila, Dkt Shadrack Opunde na Nahashon Makokha. Mzee Abdallah Mwasimba, Swila Mchiriza Sumu na Nuhu Zuberi Bakari ni kati ya washairi walioniamshia ari ya Kupenda ushairi. Namtambua Mwalimu Ayiego Ezekiel aliyenishika mkono kikamilifu.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Nikiwa mwanafunzi wa darasa la saba. Nililiwasilisha mbele ya walimu na wanafunzi wenzangu na kuzawidiwa Kamusi ya Kiswahili.

Mashairi yako huegememea zaidi mada zipi?

Matukio yanayoiathiri jamii kwa njia moja ama nyingine; hasa dini, siasa, mapenzi, ufisadi, ndoa, elimu na kadhalika.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Mara nyingi wazo nilalopania kuliandikia ndilo huchangia mada mbalimbali za mashairi yangu.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Muda hutegemea aina na urefu wa shairi husika. Ingawa hivyo, dakika 20 hivi hunitosha kutunga shairi la tarbia la hadi beti nane.

Mbona mashairi ya arudhi?

Ukweli ni kuwa mashairi ya arudhi huwa na utamu wa kipekee, humfikirisha sana mtunzi na huvutia sana yanapokaririwa au kughaniwa kwa sababu ya mdundo wa kingoma utokanao na urari wa vina.

Nini maoni yako kuhusu ushairi huru?

Mtu hawi mtu pasi kupitia hatua fulani maishani. Ndivyo yalivyo mashairi huru ambayo humpa mtunzi nafasi ya kutoa hoja zake bila vizingiti vyovyote wakati anapojifunza kutunga.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Mbali na kutuzwa vyeti vya kila sampuli, ushairi umenikutanisha na mikota mbalimbali wa lugha ndani na nje ya Kenya. Kwa njia moja au nyingine, mikota hawa wameniwezesha kupanda kwenye majukwaa mengi ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa katika ulingo wa Kiswahili. Nimetambuliwa na kutuzwa mara si haba katika makongamano mengi ya Kiswahili.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Kwa sasa ninaanda kazi ambayo naamini itawafaidi walimu na wanafunzi wengi wa Ushairi wa Kiswahili. Napania pia kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuanzisha mashindano ya mashairi katika viwango vya magatuzi ambapo washairi bora watatambuliwa na kutuzwa pakubwa.

Unakabiliana na changamoto zipi katika makuzi ya ushairi?

Ukosefu wa ufadhili na pia mtazamo hasi kuhusu Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na baadhi ya walimu.

Mbali na kutunga na kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi ni Afisa wa Polisi na mwalimu wa Kiswahili.

Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Nawashukuru watangulizi wangu kwa kutoa mwelekeo na kutuchorea ramani ya ushairi. Wazidi kutushika mikono. Chipukizi tuwe tayari kujifunza na tuepuke tabia ya kuwaiga wengine, chambilecho Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Mungu alipokuumba wewe alitaka uwe wewe! Tujikaze tu. Tutafika.