Makala

MSHAIRI WETU: Jesse Chege Mwangi almaarufu 'Malenga Mzalendo'

February 25th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

USHAIRI ni utungo unaoelezea hisia za ndani za msanii kutegemea mazingira yake. Ni utanzu ambao haujachapukiwa sana ikilinganishwa na tanzu nyinginezo za Fasihi Andishi.

Ujumbe wa shairi huwasilishwa kwa njia ya mkato na kwa lugha ya mnato yenye mdundo wa kimuziki ili kuteka hisia za msomaji au msikilizaji.

Kazi yoyote ya fasihi itavutia hadhira iwapo mtunzi atateua kutumia lugha nyepesi itakayofumbata masuala ya kawaida katika mazingira ya kila siku ya maisha ya binadamu. Haya ndiyo maoni ya mshairi Jesse Chege Mwangi almaarufu ‘Malenga Mzalendo’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Nilizaliwa mnamo 1996 katika kijiji cha Kigumo, Kaunti ya Murang’a. Mimi ni kifungua mimba katika familia ya Bw Samson Mwangi na Bi Freshiah Njeri. Kwa sasa nasomea sanaa na elimu katika Chuo Kikuu cha Egerton, Bewa la Njoro, Nakuru.

Mimi ni mpenzi ashiki wa lugha faridi ya Kiswahili na huhisi kwamba kila uchao nina wajibu mkubwa wa kutekeleza katika maenezi yake na mojawapo ni kupitia utunzi wa mashairi.

Mwalimu wangu wa shule ya upili alinipagaza jina ‘Malenga Mzalendo’ kwa sababu niliyaegemeza mashairi yangu katika utetezi wa nchi yetu dhidi ya dhuluma za ukoloni mamboleo kama ilivyo sasa.

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya Kigumo, eneobunge la Kigumo, Murang’a hadi 2011 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Kiambu, kisha St Francis Lare, Nakuru nilikofanyia mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE).

Nani na nini kilikuchochea kuupenda ushairi?

Kusoma vitabu na makala mengi kuhusu ushairi. Kusikiliza vipindi vya redio na runinga vilivyokuwa vikiongozwa na Nuhu Zubeir Bakari na Munene Nyaga pasipo kusahau kipindi cha ‘Malimwengu’ cha Lolani Kalu katika iliyokuwa runinga ya QTV.

Walipokuwa wakighani mashairi yao, Bakari na Lolani walinipa motisha sana ya kuendelea kutunga. Pia wazazi wangu, ndugu yangu (Regina), binamu (Jesse Karau) na shangazi yangu (Bi Eunice) hunitia moyo kila wakati ninapotunga.

Isitoshe, walimu wangu wa Kiswahili Bi Lucy, Bw Momanyi (St Francis Lare), Dkt Gacheiya na Dkt Taib Ali (Egerton) hunihimiza sana.

Washairi wenzangu hasa Bw Josiah, Bw Awando, Bi Mercy na Bw James Bin John pia wamenijenga pakubwa katika ulingo wa sanaa.

Nimejifunza mengi kutokana na mashairi mbalimbali ambayo huchapishwa na gazeti hili la Taifa Leo.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza

Mnamo 2012 nikiwa mwanafunzi katika shule ya upili. Shairi la kwanza lilikuwa lenye mada ‘Tuhurumie’ baada ya vita vya kikabila kuzuka kule Mto Tana kati ya Wapokomo na Waoromo.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Hujikita zaidi katika masuala ibuka katika jamii hususan ufisadi, elimu, uongozi, dini, siasa na nafasi ya mwanamke katika jamii za kisasa.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Mazingira ndicho kichocheo kikubwa zaidi. Mambo yanayoendelea katika mazingira huupa moyo msukumo wa kutaka kujieleza au kueleza jambo fulani; ili waja wapate kusikia liwe la kusifu au kukashifu.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Kwa kawaida, dakika 20 hunitosha kutunga kazi aali yenye ujumbe kamilifu huku nikizingatia sheria zote za utunzi wa mashairi ya arudhi. Hata hivyo, suala la muda hutegemea sana urefu na aina ya shairi husika.

Mbona mashairi ya arudhi?

Mashairi ya arudhi yana mnato na utaratibu wa kipekee haswa yanapotungwa vizuri kwa kuzingatia utoshelezi unaofaa wa mizani na vina huku pia leseni ya ushairi ikitumika.

Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?

Mashairi huru yana nafasi maalumu katika kupitisha ujumbe. Hivyo, watunzi wa mashairi ya arudhi (wanamapokeo) wasiwapungie kidole wenzao wanamapinduzi (huru) kwani tofauti kuu pale ni matumizi ya kanuni za utunzi tu.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Umenifanya kukutana na mabingwa katika utunzi wa mashairi kama vile Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Profesa Rocha Chimerah, Kaka Masika (Mtoto wa Salome), Bw Dominic Oigo na Bw Dancan Obwocha.

Aidha, nilizawidiwa sana na walimu wangu kwa kuwa mwanafunzi bora katika utunzi katika shule ya msingi na upili.

Nimekuwa nikihusika katika utunzi wa mashairi yanayoghaniwa katika tamasha za muziki vyuoni na kanisani.

Wanafunzi wenzangu katika Chuo Kikuu cha Egerton wanakienzi kipaji changu cha utunzi na hunitia hamasa zaidi kila mara kazi zangu zinapochapishwa gazetini.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na ushairi?

Napania kuzidi kutunga mashairi mengi na kuwa kielelezo bora kwa wengine.

ili waanze kutunga, tuuparamie utanzu huu kwa pamoja na kuwahimiza kuupenda zaidi. Naandaa diwani itakayochapishwa hivi karibuni ikiwalenga wanafunzi wa shule za msingi na upili.

Mbali na kutunga na kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi ni mwalimu na pia mtunzi wa hadithi fupi. Ninashirikiana na Kaka James Bin John kuchambua vitabu teule.

Unawashauri nini washairi chipukizi?

Wazidi kujituma na kufanya idili pasipo kufa moyo kwani safari ya utunzi ingali ndefu na i mikononi mwao. Huenda nyota zao zikawamwaia mwangaza siku za usoni.