Makala

MSHAIRI WETU: Joshua Anyona almaarufu 'Malenga Shupavu'

February 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

USHAIRI ndiyo njia nyepesi zaidi ya kuwasilisha ujumbe kuhusu masuala yanayomzunguka mwanadamu na maisha yake.

Mashairi yameelekea kupendwa na wengi zaidi hivi karibuni kiasi cha kuibua ushindani mkubwa kati ya watunzi na wale wanaoyaghani.

Mashairi au shairi huweza kubuniwa papo kwa hapo. Utunzi hauhitaji ustadi wowote ule ila lazima mtunzi awe mkwasi wa msamiati na umilisi wa lugha ili kulifanya shairi lake kuvutia. Shairi halitapendeza sana iwapo halitawasilishwa kwa ukawaida na usahili wake. Mashairi mengi yanayotumia lugha isiyo nyepesi kwa mtazamo wangu, hayapati nafasi kubwa katika ulingo wa sasa kifani.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Jina langu ni Joshua Anyona almaarufu ‘Malenga Shupavu’. Nilizaliwa miaka 21 iliyopita na kwa sasa nasomea ualimu (Historia na Kiswahili) katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA).

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya St Andrew’s Kaggwa Boys Nyansiongo, Kaunti ya Nyamira kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Tengecha Boys, Kericho.

Nani na nini kilichokuchochea kuupenda ushairi?

Kusikiliza nyimbo za Taarab na kusoma vitabu na makala mengi ya Kiswahili. Kuwasikiliza malenga wengine wakighani mashairi yao kulinitia motisha sana. Pia walimu wangu wa shule za upili na marafiki zangu wa tangu kitambo kama vile Josephat Mironga na Bi Benta Vusha walinihimiza na kunikuza mno kisanaa.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Nilitunga shairi langu la kwanza lenye anwani ‘Tawahudi’ nikiwa mwanafunzi wa kidato cha nne mnamo Oktoba 18, 2015. Lengo kuu la shairi langu lilikuwa ni kuwapa walemavu motisha na ari ya kuishi huku nikiwahimiza wanajamii wengine kutowabagua.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Huzamia sana katika kujadili masuala ya ulemavu, siasa, athari za mapenzi na mimba za mapema.

Nini hukuongoza kuteua mada hizo?

Mazingira na masuala ibuka katika jamii na matukio ya kawaida yanayomkabili wanadamu katika mazingira yake.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Muda wa dakika nne hadi sita hivi hunitosha kutiririsha shairi la tarbia lenye beti tano au sita.

Mbona mashairi ya arudhi?

Mashairi ya arudhi hufuata sheria, kaida na taratibu zote za utunzi. Hivyo, huwa ni rahisi sana kutunga na kuyaghani.

Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?

Huandikwa bila ya kufuata sheria zozote za utunzi. Waandishi wanaoasi arudhi zinazoongoza utunzi wa mashairi huitwa wanamapinduzi. Mashairi huru hutambuliwa kwa kusoma au kuangalia sura ya nje (muundo). Mashairi haya yasiyofuata arudhi husisitiza sana umuhimu wa ujumbe uliomo.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Umeniwezesha kukichapukia Kiswahili zaidi, kuimairisha msamiati wangu, kutangamana na walimu stadi na baadhi ya malenga shupavu zaidi nchini. Isitoshe, nimezawidiwa katika tamasha mbalimbali za muziki na katika makongamano mengi ya makuzi ya lugha. Wanafunzi wenzangu katika Chuo Kikuu cha CUEA pia wamenitambua pakubwa kutokana na kipaji changu cha utunzi.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusiana na makuzi ya ushairi?

Ninapania kuandika mashairi kwa wingi na kuchapisha diwani ili kazi zangu zisomwe na wapenzi wengi wa mashairi hasa walimu na wanafunzi wa shule za upili.

Mbali na kutunga (au) kughani mashairi, unafanya nini kingine?

Mimi ni mwalimu na pia mwanachama wa kundi la ‘Naftunes Production’ ambalo limepania sana kuwalea wapigaji picha, wanafilamu na watunzi wa muziki.

Unawashauri nini chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Waendelee kukuza fani ya ushairi kwa kutunga zaidi kuhusu mambo ambayo yanatuelekeza kimaadili.