Makala

MSHAIRI WETU: Wangu Kanuri almaarufu 'Malenga wa Baraka'

August 14th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

USHAIRI ni kioo cha jamii kinachopania kumulika masuala ibuka katika jamii na masaibu ya mara kwa mara katika maisha ya kila siku ya binadamu.

Zaidi ya kuonya, kukejeli, kupongeza, kutoa wosia na kuburudisha, ushairi pia hutumiwa kuelimisha na kuipa jamii mwelekeo.

Ushairi utungwao kwa picha humsaidia mtunzi kuangazia mambo tofauti yanayoihusu jamii yake.

Dhana hii ambayo haijakuzwa sana, huvutia mno kwani mshairi ana uwezo wa kuwasilisha mawazo ya sampuli nyingi bila ya kujifunga kwa mada moja maalumu.

Huu ni mtazamo wa mshairi Wangu Kanuri almaarufu ‘Malenga wa Baraka’.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Mimi ni mwanafunzi wa Shahada ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Daystar. Napenda sana kusoma kazi mbalimbali za Kiswahili, kuandika kazi za kibunifu, kushona na kupika. Mimi pia ni mhariri wa Kiswahili katika Jarida la Involvement chuoni Daystar.

Ulisomea wapi?

Katika Shule ya Msingi ya Thika Bell House Academy, Kaunti ya Kiambu kisha Master Education Centre iliyoko Kutus, Kaunti ya Kirinyaga kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Naromoru Girls katika Kaunti ya Nyeri.

Nini kilikuchochea kuupenda ushairi?

Kivutio kikubwa zaidi ni mdundo wa kingoma utokanao na urari wa vina kwenye mishororo ya shairi. Pili, ni uhuru wa utunzi ambao mara nyingine hunipa jukwaa la kuficha ujumbe katika mafumbo. Utunzi ni kipaji ambacho Mungu amenitunuku nacho; nami napania sana kukitumia kuwazindua wanajamii na kujibu mengi ya maswali ambayo wao hujiuliza mara kwa mara.

Ulitunga lini shairi lako la kwanza?

Mnamo Machi 2016. Lilikuwa na ujumbe wa pongezi kwa akina mama ambao siku zote wana majukumu makubwa na mazito katika jamii. Shairi lenyewe lilikuwa na makosa mengi kwa kuwa halikuzingatia kanuni muhimu za utunzi.

Mashairi yako huegemea zaidi mada zipi?

Huzamia masuala yenye uwezo wa kuzua majonzi na furaha kwa viwango sawa. Licha ya mengi ya mambo ninayoyajadili kuwa ya kawaida tu, najaribu sana kuzingatia ubunifu wa hali ya juu.

Unahitaji muda kiasi gani kutunga shairi moja?

Dakika 45 hivi hunitosha kutunga shairi la tarbia la kati ya beti sita na nane. Ingawa hivyo, urefu au ufupi wa muda hutegemea pia mazingira na uzito wa mada husika.

Mbona mashairi ya arudhi?

Kuzingatiwa kwa arudhi hudumisha urari ambao hufanya shairi kuwa la kuvutia kila linaposomwa au hata kusikilizwa. Zaidi ya kulipa shairi mnato, arudhi hufanya mashairi kuimbika kwa wepesi na ndicho kipimo kamili cha ukomavu wa mtunzi.

Nini maoni yako kuhusu mashairi huru?

Huwa ni jukwaa la chipukizi wanaojifunza utunzi kupanga mawazo yao kwa utaratibu ufaao kabla ya kumudu kutunga mashairi ya arudhi.

Ushairi umekuvunia tija ipi?

Nimewahi kuangaziwa kwenye vipindi mbalimbali vya makuzi ya sanaa katika vituo vya Radio Citizen (Mseto Extra), KU-TV (Arts and Culture), Y-254 (E-Circuit) na Focus TV.

Weledi wangu katika ushairi uliwahi kufanya nichaguliwe Mwenyekiti wa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Naromoru Girls na pia kunipa fursa ya kutafsiri kitabu ‘Save the Elephants’ chake Dkt Lucy King.

Una mipango ipi ya baadaye kuhusu ushairi?

Nalenga kuchapisha diwani itakayowasaidia sana walimu na wanafunzi wa shule za upili kuizamia fani ya ushairi kwa wepesi zaidi.

Unawashauri nini washairi chipukizi na watangulizi wako kitaaluma?

Chipukizi wasikate tamaa. Wavute subira na wajifunze kutoka kwa watunzi wa zamani ambao ninawahimiza wazidi kutushika mikono.