AREGE RUTH Na ABDULRAHMAN SHERIFF
BAO la mshambulizi Fasila Adhiambo dhidi ya Gusii Starlets, limewapa wanajeshi wa Ulinzi Starlets matumaini ya kuendelea kutetea taji lao wakati wa mechi za raundi ya 32 ya kombe la wanawake la Shirikisho la Soka nchini (FKF) ambayo ilichezwa ugani Gusii katika Kaunti ya Kisii mnamo Junamosi.
Adhiambo ambaye alijiunga na timu hiyo mapema mwezi huu, alicheka na wavu dakika za lala salama kipindi cha kwanza.
Timu ya Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL) Kayole Ladies, imeona vimulimuli mikononi mwa Falling Waters Barcelona ambao waliwanyorosha 4-3 ugani Camp Toyoyo jijini Nairobi.
Mabao ya Kayole yalitiwa kimiani na Veronica Dunge, Bilha Osong dakika ya 58 na 72 mtawalia naye beki Pauline Achuka akawapa wageni zawadi kwa kujifunga bao dakika ya 46.
Washambulizi wa Barcelona Jane Njeri na Calta Masinde walifunga mabao mawili kila mmoja. Naye Naomi Masinde akafunga penalti dakika ya sita.
Kwingineko, klabu mbili kutoka ukanda wa Pwani, Mombasa Olympic Ladies na Fortune Ladies FC pia zilifuzu kuingia kwenye raundi ya 16.
Mombasa Olympic iliweza kuishinda Coast Starlets FC kwa bao 1-0 katika uwanja wa shule ya msingi ya Ronald katika shindano hilo la maondoano linalofanyika kwa mara ya kwanza.
Katika mechi hiyo kali ya debi ya timu za Pwani ambazo zinashiriki Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Mombasa Ladies ilijipatia bao lao la ushindi kunako dakika ya sita mfungaji akiwa Happy Mutta.
Kocha wa Mombasa Ladies FC Cristine Nanjala amesema wamefurahikia ushindi huo kwani wachezaji waliocheza wengi walikuwa wamepewa nafasi kucheza kwa ajili ya kuwapumzisha wale ambao wamecheza mechi nyingi za ligi.
“Tumewapa nafasi wachezaji ambao hawachezi mechi nyingi za ligi na wameonyesha kuwa nao pia wanaweza kusaidiana na kupumzishana na wanasoka ambao wanacheza mechi nyingi za ligi tunayoshiriki,” akasema Nanjala.
Naye mkufunzi wa Coast Starlets FC Hashim Faraj amewasifu wanasoka wake kwa jinsi walivyocheza kwa kujitolea lakini akamlaumu mwamuzi kwa kuonyesha mapendeleo yaliyosababisha kushindwa kwao.
“Tumepoteza mechi sababu ya uchezeshaji mbaya,” akadai Faraj.
Nayo Fortune Ladies FC ilifanikiwa kwa mara ya pili kupata ushindi wa bwerere baada ya wapinzani wao kutoka Nyanza, Gideon Starlets kushindwa kufika uwanja huo wa RG Ngala kwa mechi yao.
Matokeo mengine;
Gusii Starlets 0-1 Ulinzi Starlets
Kangemi Ladies 1 (3)- 1 (4) Soccer Sisters
Sunderland Samba 0- 1 Kisped Queens
Kayole Starlets 3-5 Falling Waters Barcelona
Coast Starlets 0- 1 Mombasa Olympic
Fortune Ladies 1 (5) – 1 (6) Gideon Starlets
Young Bullets 1- 6 Nakuru City Queens
Kapsabet Starlets 0 – 5 Kibera Girls Soccer
University of Eldoret (UoE) 0-5 Eldoret Falcons