Habari Mseto

Mshangao huku wakazi wakiua 'mabaunsa' 6 mazishini

November 17th, 2019 2 min read

NA MWANDISHI WETU

MAZISHI ya mfanyabiashara katika Kaunti ya Busia yaligeuka uwanja wa maangamizi wakati waombolezaji waliposhambulia na kuua vijana sita.

Katika kisa hicho cha usiku wa kuamkia jana, waombolezaji katika kijiji cha Masebula, Kaunti ya Busia walivamia vijana hao ikidaiwa walidhani ni wahalifu waliohusika katika mauaji ya mfanyabiashara mashuhuri, Johanes Okoth aliyeuawa kwa kupigwa risasi.

Baadaye, ilibainika vijana hao ambao baadhi yao ni wenye miraba minne, walikuwa miongoni mwa kundi la ‘mabaunsa’ kumi waliopewa kazi ya ulinzi na mmoja wa jamaa za marehemu.

Wanaboda boda walijumuika na waombolezaji kuwavamia sita hao waliovalia mavazi meusi.

Walioshuhudia kisa hicho ambacho kimeshangaza wengi walisema, waathiriwa walikataa kujitambulisha walipoambiwa wafanye hivyo, maadamu hawajulikani eneo hilo kwa kuwa walikodishwa kutoka Kaunti ya Kisumu.

Duru zilisema polisi walimkamata mmoja wa wake za marehemu ili kumhoji kwa kuwa ilisemekana yeye ndiye aliwaleta.

“Watu 10 waliovalia suti nyeusi walikuwa katika msafara wa mazishi kutoka mochari ya Hospitali ya Misheni Sega ambapo tulikuwa tumeenda kuchukua mwili wa kakangu. Tulipowasili nyumbani, tuliwataka wajitambulishe kwa sababu walikuwa wageni,” alisimulia Bi Roselyne Aduol, dadake marehemu mfanyabiashara huyo.

“Wote walikataa kujitambulisha jambo lililowakasirisha waombolezaji wale wengine waliowavamia kwa rungu. Wanne walifanikiwa kutoroka,” alisema Bi Aduol. Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Kaunti ya Busia Bw Jacob Narengo alisema kuwa habari zilizokusanywa na polisi ziliashiria kuwa wenyeji waliingiwa na shaka baada ya mwanamme mmoja kuonekana akizunguka kwa njia ya kutiliwa shaka akiwa amebeba mkoba mweusi.

“Wenyeji ambao walirekodi taarifa katika kituo cha polisi walisema mmoja wa wanaume waliovalia suti nyeusi alionekana akiweka mkoba mweusi kwenye gari la kubebea jeneza na baada ya kukaguliwa, mkoba huo ukapatikana kuwa na mjeledi na visu vitatu. Hapo ndipo waombolezaji walipowashambulia baada ya kushuku kwamba walihusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo,” alisema Bw Narengo.

Bw Narengo alithibitisha kuwa waombolezaji kadha walikuwa wameandikisha taarifa katika Kituo cha Polisi cha Busia.

Hata hivyo, alilaani kitendo hicho akikitaja kuwa ukiukaji wa sheria. Miili hiyo sita ilipelekwa katika mochari ya hospitali ya kaunti Busia huku polisi wakitumwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo marehemu.