Habari MsetoKimataifa

Mshangao watoto wa miaka 9 na 6 kufunga ndoa

April 7th, 2019 2 min read

Na PHILIP WAFULA

WAKAZI wa kijiji cha Nakapyata, Baraza la Mji wa Buyende, Wilaya ya Buyende mashariki mwa Uganda, wamestaajabisha wengi kwa kufunganisha ndoa ya watoto wawili.

Harusi hiyo ya kitamaduni iliandaliwa kati ya mvulana mwenye umri wa miaka tisa, na ‘mke wake’ aliye na umri wa miaka sita.

Mvulana huyo, ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Nne katika Shule ya Msingi ya Buyende Light na msichana, ambao wote walisemekana walizaliwa wakiwa na meno mawili, walifanya harusi wiki iliyopita na kupewa chumba watakamoishi pamoja.

Katika sheria za Uganda, ni haramu kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 18 kuozwa au kushiriki ngono.

Ilidaiwa watoto hao walianza ‘kuchumbiana’ wakati mvulana alipokuwa mwenye umri wa miaka mitatu na msichana alikuwa na miezi mitatu pekee.

“Mwanangu alizaliwa akiwa na meno mawili na mke wake pia alizaliwa hivyo. Kuzaliwa kwake kulileta baraka tele na tunatarajia jina lake litaleta umoja kwa makabila ya Baganda na Basoga,” akasema babake mvulana huyo.

Barbra Namulesa, ambaye ni mwalimu wa mvulana huyo, alimtaja kama mvulana mpole, mwenye nidhamu na anayeshirikiana sana na wenzake na pia huongea kama mzee.

“Nadhani huyu ndiye Kintu (anayeaminika kuwa baba wa kwanza ulimwenguni katika jamii ya Baganda) ambaye mababu wetu walihadithia. Yeye hunishauri hata licha ya kuwa mimi ndiye mwalimu wake,” akasema.

Mamake msichana alisema binti yake amekuwa wa kipekee tangu alipozaliwa.

“Alianza kuzungumza mara alipozaliwa. Wakati nilipojifungua niliuliza mtoto wangu ni wa jinsia gani nikaambiwa ni wa kike. Lakini nilishangaa mkunga aliponiambia mtoto amezaliwa akiwa na meno mawili, karibu nimwangushe,” akasema mama huyo wa watoto saba, akieleza alivyohofia kumnyonyesha akiwa na meno.

Katika harusi hiyo ambayo ilijaa nyimbo na densi, baadhi ya waliohudhuria walizirai baada ya kuona mvulana huyo na msichana wameketi kando ya nyoka wawili wenye urefu wa futi tatu kila mmoja. Wazee walidai nyoka hao walinuiwa kulinda ‘wanandoa’ hao.

Msemaji wa polisi katika eneo la Busoga Kaskazini, Michael Kasadha alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

“Ndoa yoyote inapaswa kuwa kati ya watu wenye umri wa miaka 18 kuendelea. Tunataka kubainisha ukweli kuhusu hayo yaliyotokea,” akasema.