Habari MsetoSiasa

Mshauri wa Raila, Silas Jakakimba asakwa Zimbabwe kwa 'kuchochea ghasia'

August 7th, 2018 2 min read

VALENTINE OBARA na BARACK ODUOR

POLISI wa Zimbabwe wanamtafuta msaidizi wa Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, kwa madai kuwa alichochea ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa urais nchini humo wiki iliyopita.

Mashirika ya habari Zimbabwe yalimnukuu Msemaji Mkuu wa polisi, Bi Charity Charamba, akisema wanataka kumhoji Bw Silas Jakakimba kuhusiana na ghasia hizo zilizotokea wakati upande wa upinzani ulipinga matokeo ya uchaguzi.

Katika uchaguzi huo, Rais Emmerson Mnangagwa wa chama cha ZANU-PF alitangazwa mshindi dhidi ya Bw Nelson Chamisa wa chama pinzani cha Movement for Democratic Change (MDC).

“Wananchi wanaojua aliko wanaombwa kuwasiliana na idara ya upelelezi wa jinai au kuripoti kwa kituo chochote cha polisi kilicho karibu nao,” akasema Bi Charamba.

Bw Jakakimba ni mmoja wa wandani wa kisiasa wa Bw Odinga na amekuwa akiandamana naye kwa ziara mbalimbali zikiwemo za mataifa ya kigeni mbali na kuwa kati ya wanaompangia kigogo huyo wa kisiasa mikakati yake.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Jakakimba alithibitisha aliwahi kuhudhuria mkutano wa hadhara wa MDC wakati wa kampeni lakini hakuwa mpangaji mikakati wa chama hicho wala wa Bw Chamisa.

Katika mkutano huo wa hadhara uliokuwa wa mwisho jijini Harare, Bw Chamisa alimtambulisha kama mwakilishi wa Bw Odinga ambaye chama chake cha ODM kimekuwa mshirika wa karibu wa MDC kwa miaka mingi.

Akizungumza kutoka bomani kwake katika kijiji cha Kakimba, Kisiwa cha Mfangano, Kaunti ya Homa Bay, alisema alikuwa Harare kwa siku tatu akaondoka Jumanne iliyopita na kurejea Nairobi kabla ghasia zianze kushuhudiwa Zimbabwe.

“Nilipotoka Harare hali ilikuwa tulivu na shughuli zilikuwa zikiendelea kama kawaida,” akasema.

Chama cha MDC kilipinga matokeo ya uchaguzi wa urais na kudai kulikuwa na ulaghai.

Kabla tume ya uchaguzi nchini humo kutangaza matokeo, wagombeaji hao wawili walikuwa kila mmoja akitangaza kuongoza kwa idadi ya kura na hali hii ilisababisha taharuki nchini humo.

Ilibidi wanajeshi na polisi kutumiwa kutawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakiandamana na watu kadha wakauawa kwenye makabiliano hayo.