Michezo

Mshindi kati ya Gor na Ingwe kuumiza nyasi dhidi ya Hull City Mei 13

April 24th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Hull City ya Uingereza itapambana na mshindi kati ya wapambe wa ligi Gor Mahia na AFC Leopards katika mechi inayotarajiwa kusakatwa Mei 13, 2018.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Klabu ya Hull City inayoshiriki kwenye ligi ya daraja la pili kucheza mechi dhidi ya wachezaji kutoka taifa letu.

Mwaka wa 2017 timu hiyo ilivaana na kikosi cha KPL All Stars  na kushinda kwa mabao 2-1.

Kikosi cha Hull City kinatarajiwa kutua hapa nchini Mei 11 kwa maandalizi ya mechi inayosubiriwa kwa hamu na ghamu na wapenzi wa soka hapa nchini.

Hata hivyo kutachezwa soka ya kusisimua kati ya watani wa tangu jadi Gor Mahia na AFC Leopards Mei mosi uwanjani Afraha Kaunti ya Nakuru. Mshindi katika mtanange huo atakuwa na fahari na tija ya kukutana na kikosi cha Hull City.

Katibu katika Wizara ya Michezo Kirimi Kaberia amewapa matumaini wapenzi wa soka kwamba uwanja wa kimaitaifa wa Moi Kasarani utakuwa tayari na utatumika kuandaliwa kwa mechi hiyo kubwa.

“Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba uwanja wa Kasarani ambao umekuwa ukikarabatiwa unakuwa tayari kabla ya siku ya mchuano huo. Tutazuru uwanja huo kukagua hali lakini kufika mwezi Juni mwaka 2018 lazima shughuli za ukarabati ziwe zimeisha,”  akawaambia wanahabari.

Nyanja za Nyayo na Kasarani zimekuwa zikifanyiwa ukarabati na Klabu nyingi zinazoshiriki KPL zimekuwa zikitatizika kuhusu nyanja za kuchezea mechi za ligi.