Mshindi wa EPL msimu huu huenda akapatikana katika wiki ya mwisho – Pep Guardiola

Mshindi wa EPL msimu huu huenda akapatikana katika wiki ya mwisho – Pep Guardiola

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amesema huenda mshindi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu akapatikana katika wiki ya mwisho.

Kwa mujibu wa mkufunzi huyo raia wa Uhispania, kampeni za EPL muhula huu zitarejesha kumbukumbu za 2018-19 ambapo waajiri wake Manchester City walitwaa ubingwa wa EPL baada ya kupiku Liverpool kwa alama moja pekee.

Man-City walinyanyua pia taji la EPL mnamo 2013-14 kwa alama 86, mbili pekee kuliko Liverpool walioambulia nafasi ya pili. Kufikia sasa, Man-City waliojizolea alama 98 mnamo 2018-19, wanajivunia pointi 83, moja pekee kuliko nambari mbili Liverpool ambao pia wametandaza michuano 34.

Baada ya kurudiana na Villarreal kwenye nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 3, 2022, Liverpool wanaowania mataji manne msimu huu, wataalika Tottenham Hotspur kisha kuendea Aston Villa ligini kabla ya kukwaruzana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 14 ugani Wembley. Watafunga msimu kwa michuano miwili ya EPL dhidi ya Southampton na Wolves mtawalia.

Kwa upande wao, Man-City watamenyana na Real Madrid kwenye mkondo wa pili wa UEFA mnamo Mei 4, 2022 nchini Uhispania kabla ya kutamatisha kampeni za EPL dhidi ya Newcastle, Wolves, West Ham na Aston Villa kwa usanjari huo.

“Tutarajie ushindani mkali hadi wiki ya mwisho. Sawa na Liverpool, sisi pia tuna azma ya kuhifadhi taji la EPL. Liverpool wameweka wazi malengo yao mengine ya kupigania mataji manne msimu huu. Mabadiliko kwenye msimamo wa jedwali la EPL mwishoni mwa muhula yatakuwa madogo mno,” akasema Guardiola.

“Sijui kitakachofanyika katika wiki mbili zijazo. Bado ni mapema sana kubashiri mshindi wa EPL. Hata hivyo, maazimio yetu yako wazi – tunalenga ubingwa wa makombe kadhaa na tunaomba mashabiki wavute subira,” akasema kocha Jurgnen Klopp.

Liverpool ambao ni mabingwa hao mara 19 wa EPL, walipepeta Villarreal 2-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA mnamo Aprili 27, 2022 ugani Anfield. Walitawazwa wafalme wa Carabao Cup mwishoni mwa Februari baada ya kufunga Chelsea penalti 11-10 na watavaana na kikosi hicho kwenye fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Mei 14.

Tofauti na Villarreal waliopigwa 2-1 na Alaves wikendi iliyopita katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Liverpool watajitosa ulingoni dhidi ya kikosi hicho cha kocha Unai Emery wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle United katika pambano lililopita la EPL.

Japo Liverpool wanapigiwa upatu wa kuteremkia Villarreal, kibarua kinachowasubiri si chepesi. Juventus na Bayern Munich wote walishindwa kuangusha masogora wa Emery katika UEFA uwanjani La Ceramica muhula huu. Isitoshe, Villarreal hawajapoteza mechi yoyote kati ya 12 zilizopita katika uwanja wao wa nyumbani tangu Novemba 2021.

Ni kikosi kimoja pekee ambacho kimewahi kubatilisha kichapo cha zaidi ya mabao mawili kwenye nusu-fainali ya UEFA na kutinga fainali. Klabu hiyo ni Liverpool iliyopepeta Barcelona 4-0 katika marudiano licha ya kupoteza mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya 2018-19 kwa 3-0.

Iwapo Liverpool watafuzu kwa fainali ya UEFA msimu huu, basi watajiweka katika kundi moja na Real (16), Bayern (11) na AC Milan (11) ambao wamewahi kunogesha fainali ya kivumbi hicho zaidi ya mara 10.

Mchuano dhidi ya Newcastle ulikuwa wa tano mfululizo kwa Liverpool kushinda katika mashindano yote. Walikamilisha mechi nne kati ya hizo bila kufungwa bao na hawajahi kupoteza pambano lolote ugenini tangu Disemba 2021 Leicester City iwakung’ute 1-0 ugani King Power.

Rekodi hiyo imewashuhudia wakishinda michuano yote mitano ya ugenini katika UEFA msimu huu huku wakifunga angalau mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi hizo. Liverpool walipigwa 1-0 walipokutana na Villarreal mara ya mwisho ugani La Ceramica kwenye nusu-fainali ya Europa League mnamo 2015-16.

Bao jingine kwa fowadi Sadio Mane wa Liverpool leo litamshuhudia akifikia rekodi ya Frank Lampard aliyewahi kupachika wavuni mabao 15 katika nusu-fainali za UEFA akivalia jezi za kikosi kinachoshiriki soka ya EPL (Chelsea).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nassir na Omar walenga wawaniaji wenza wa kike

SHINA LA UHAI: Vidimbwi vya chumvi vyavuruga wanakijiji

T L