Mshindi wa Ligue 1 msimu huu kujulikana siku ya mwisho ya kampeni

Mshindi wa Ligue 1 msimu huu kujulikana siku ya mwisho ya kampeni

Na MASHIRIKA

NI rasmi kwamba mshindi wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu wa 2020-21 sasa atajulikana katika siku ya mwisho ya kampeni za kipute hicho.

Hii ni baada ya viongozi wa jedwali Lille kulazimishiwa sare tasa na Saint-Etienne mnamo Jumapili na hivyo kuruhusu Paris Saint-Germain (PSG) waliowaponda Reims 4-0 kupunguza pengo la alama kati yao hadi pointi moja pekee.

Lille ambao kwa sasa wanajivunia alama 80, wangatwaa taji la Ligue 1 iwapo wangaliwashinda St-Etienne uwanjani Stade Pierre Mauroy.

Reims walilazimika kucheza dhidi ya PSG kwa zaidi ya dakika 80 wakiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani baada ya Yunis Abdelhamid kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kunawa mpira ndani ya kijisanduku. Tukio hilo liliwapa PSG motisha tela na wakafungiwa mabao mawili ya kwanza kupitia Neymar na Kylian Mbappe katika dakika za 13 na 24 mtawalia.

Marquinhos Correa na Moise Kean waliongoza PSG kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao katika gozi hilo lililochezewa ugani Parc des Princes.

Lille waliopoteza nafasi nyingi za wazi dhidi ya St-Etienne, sasa watakamilisha kampeni zao za Ligue 1 muhula huu dhidi ya Angers mnamo Mei 22. Kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino atawaongoza waajiri wake PSG kupepetana na nambari 16 Brest siku hiyo.

AS Monaco watakaochuana na Lens katika mechi ya mwisho msimu huu, pia wana fursa ya kujitwalia taji la Ligue 1. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya tatu kwa alama 77 baada ya kupokeza Rennes kichapo cha 2-1 mnamo Jumapili.

Bao ambalo Mbappe alifungia PSG dhidi ya Reims lilikuwa lake la 40 katika mapambano yote ya msimu huu na la 26 kufikia sasa ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Borussia Dortmund waendeleza ufufuo wao kwenye Bundesliga...

AC Milan watoka sare dhidi ya Cagliari kwenye Serie A