Mshindi wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Hegerberg, arejea ulingoni baada ya jeraha kumweka nje kwa miezi 20

Mshindi wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Hegerberg, arejea ulingoni baada ya jeraha kumweka nje kwa miezi 20

Na MASHIRIKA

MSHINDI wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Ada Hegerberg wa Olympique Lyon, amesema hatawahi kuchukulia soka kama suala la kimzaha baada ya kupona jeraha lililomweka mkekani kwa kipindi cha miezi 20 iliyopita.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amejumuishwa katika kikosi kinachojiandaa kuvaana na BK Hacken ya Uswidi kwenye mechi ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 5, 2021.

Hegerberg ambaye ni raia wa Norway, hajatandaza soka katika mchuano wowote tangu Januari 2020 baada ya kupata jeraha baya la misuli ya mguu.

“Nimekomaa vilivyo kama mwanamke na mwanasoka. Nimejifunza mengi ambayo yananipa nguvu ya kujituma ipasavyo kwa kipindi cha miaka kadhaa ijayo kitaaluma,” akasema Hegerberg.

Sogora huyo alitawazwa malkia wa Ballon d’Or katika makala ya kwanza ya tuzo hiyo kwa wanawake mnamo 2018.

Hegerberg alisaidia Lyon kunyanyua mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara nne mfululizo. Lyon ambao ni miamba wa soka nchini Ufaransa walitia kapuni taji jingine la UEFA mnamo 2019-20 baada ya Hegerberg kupata jeraha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Liverpool, Manchester City nguvu sawa ligini

Kafyu yasaidia kuepusha hali mbaya shughuli ya utoaji...