Mshtakiwa ageuzwa shahidi katika kesi ya ukwepaji ushuru

Mshtakiwa ageuzwa shahidi katika kesi ya ukwepaji ushuru

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Jumatano alifutilia mbali kesi dhidi ya mshtakiwa mwenza bilionea Humphrey Kariuki ya ukwepaji kulipa ushuru wa Sh41bilioni na kupatikana na mali ambayo haijalipiwa ushuru.

Akiwasilisha barua ya kutamatisha kesi hiyo, kiongozi wa mashtaka Bi Carol Sigei alimweleza hakimu mkuu Bi Martha Mutuku kuwa “ Bw Stuart Gerald Herd atakuwa shahidi mkuu katika kesi dhidi ya Bw Kariuki na washtakiwa wengine wanane.”

Bi Sigei alimweleza hakimu kuwa kesi dhidi ya Bw Herd itatamatishwa chini ya Sheria nambari 87(a) cha sheria za uhalifu (CPC) kifungu cha 75 cha sheria za nchi hii.

Bi Sigei alimkabidhi Bi Mutuku nakala ya barua hiyo iliyokuwa imepigwa chapa cha afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP) na kupigwa muhuru wa Feburuari 24, 2021.

Lakini ombi hilo lilizua mjadala mkali kutoka kwa mawakili wanaowatetea Bw Kariuki na washtakiwa wengine.

Wakiongozwa na wakili Cecil Miller , mawakili hao walilalamika kuwa “DPP amekaidi agizo la mahakama yam waka uliopita kwamba awakabidhi nakala za ushahidi wote katika kesi hiyo ya ukwepaji kulipa ushuru.”

Wakili Odero Osiemo alisema DPP haihataji kushauriwa jinsi ya kufanya kazi. PICHA / RICHARD MUNGUTI

Bw Miller alisema mnamo 2019 DPP alitoa taarifa kwamba amekagua ushahidi uliowasilishwa na wachunguzi na kupata kuna makosa yalitendeka ndipo akamshtaki Bw Herd, Mr Kariuki, Mabw Mr Kariuki, Mr Robert Githinji, Mr Geoffrey Kaaria Kinoti, Mr Peter Njenga, Mr Simon Maundu, Mr Kepha Githu Gakure , na Wow Beverages Limited (WBL).

Bw Herd alikuwa mmoja wa wakurugenzi wa ASL na WBL zinazotengeneza pombe kali na vinywaji vinginevyo.

“Kwa lugha rahisi hii mahakama ilimwamuru DPP atukabidhi ushahidi wote lakini akakaidi hiyo amri.Badala ya kutupa ushahidi sasa amewasilisha barua ya kutamatisha kesi dhidi ya mshtakiwa mmoja,” alisema Bw Miller.

Wakili huyo alimsihi hakimu amwamuru DPP awakabidhi ushahidi aliotegemea kuwafungulia mashtaka washtakiwa na ule aliotegemea kumwondolea Bw Herd kesi.

Bw Miller alilalamika “DPP alikaidi agizo la kutupa nakala za ushahidi.”

Lakini wakili Odero Osiemo anayemwakilisha Bw Herd katika kesi hizo tatu dhidi yao alipinga mawasilisho ya mawakili hao akisema “hakuna mtu au asasi inapasa kumwelekeza DPP atakavyotenda kazi yake.”

Hakimu mkuu Bi Martha Mutuku…Picha/ RICHARD MUNGUTI

Bw Osiemo alisema tayari DPP ameamua atatatamisha kesi dhidi ya Bw Herd na “ washtakiwa wenzake hawapasi kukataa akiondolewa mashtaka.”

“Washtakiwa hawa wanataka ushirika wa Bw Herd hapa kortini,”alisema Bw Osiemo.

Bi Mutuku aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 19 atakapopokea mawasilisho ya kila mmoja kuhusu ombi la “kumshurutisha DPP awakabidhi ushahidi aliotegemea kufikia uamuzi wa kuwashtaki Bw Kariuki na wengine na ule aliofikia kumgeuza mshtakiwa shahidi.”

Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 280 idadi jumla...

Kesi ya ufisadi ya Obado na wanawe kuendelea Nairobi