Mshtakiwa ajifungia chooni akiogopa kujua hukumu

Mshtakiwa ajifungia chooni akiogopa kujua hukumu

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa kampuni  moja inayotengeneza mvinyo na inayohusishwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga, alisababisha kioja katika mahakama ya Milimani Nairobi Ijumaa alipojifungia ndani ya choo na kukatalia mle ndani akiogopa kusikia uamuzi wa kesi aliyoshtakiwa pamoja na waajiri wake ya kuiba bidhaa za kampuni hiyo.

Hata hivyo Alex Kabaka Odera alikuwa na bahati ya mtende kwa vile yeye , wakurugenzi wawili wa kampuni ya Patialla Distillers Ltd na wafanyakazi wenzake sita waliachiliwa huru na hakimu mkuu Francis Andayi.

Bw Odera alikuwa amejifungia ndani ya choo kwa muda wa saa mbili huku akibembelezwa atoke kwa vile alikuwa anachelewesha kesi.

Hatimaye alitoka chooni lakini alikuwa anayumbayumba kutokana ulevi na harufu mbaya ya choo. Bw Odera alishikwa mkono na kuongozwa hadi kizimbani na afisa wa polisi aliyekuwa amevalia sare za umma. “Keti hapo hadi wakati ule utakaposikia jina lako likiitwa,” wakili aliyemwakilisha Odera alimwamuru.

Punde tu Odera alipotulia kizimbani huyoooo alibebwa na usingizi akalala fofofo. Kwa muda wa zaidi ya saa moja kabla ya Bw Andayi kuingia kortini Odera alikuwa anang’orota.

Kabla ya kufungua mlango wa choo na kutoka wakili Kirathe Wandugi aliyekuwa anawakilisha wakurugenzi wa Patialla Distillers Bi Mary Waigwe Muthoni na Bw Francis Kiambi alikuwa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya Odera.

“Huyu Odera amejifungia ndani ya choo. Sasa zimepita dakika 40 ikielekea saa moja. Tutafanyaje na hakuna mwenye ufunguo?” Bw Kirathe alilia.

Bw Odera aliyekuwa amelewa chakari hakufuata uamuzi uliosomwa na Bw Andayi. “Amka kesi imeisha. Toka kizimbani,” washtakiwa wenzake walimwagiza.

Alikuwa ameshtakiwa pamoja na Salim Nyakundi Masea, Joseph Njenga Thimwa, Gabriel Gitonga Njue,Patrick Mwangi Wanyoike, Danson Irungu Maina, Maurice Muiruri Wainaina, John Mayenga Ongechi, John Githuku Gathari na Hilary Kimutai Kiprop.

Nyakundi na Njenga walipatikana na kesi ya kujibu na watajitetea Februari 10,2021. Naye John Mayenga Ongechi alitoroka na Bw Andayi aliamuru dhamana aliyokuwa amelipa itwaliwe na serikali.

Lakini wale wengine tisa watarudishiwa dhamana walizokuwa wamelipa ndipo wafanye kesi akiwamo Bw Odera. Nje ya Mahakama Bw Odera aliyeonekana mwenye wasiwasi aliuliza, “kwani kumeendaje?”

Alijibiwa na wenzake, “Tumeachiliwa. Wewe ulikuwa umelala. Wacha ulevi huu wa kupindukia utakutumbukizia nyongo.”

Washtakiwa hao 12 walikuwa wamekabiliwa na shtaka la kuingiza nchini lita 100,000 za ethanol inayotengeneza mvinyo mkali.

Pembenjeu hiyo ilikuwa inapelekwa kwa kampuni moja mjini Mwanza Tanzania kutoka kwa kampuni inayohusishwa na Bw Odinga ya Kenya Spectre International Limited.

Kampuni hii pia ndiyo hutengeneza mitungi ya kuweka gesi ya kupikia. Nyakundi na Njenga waliokuwa madereva wa malori yaliyokuwa yanasafirisha ethanol hiyo walishtakiwa kuvuruga mitambo ya kodi na kupelekea serikali kupoteza kodi ya Sh20,450,000.

You can share this post!

Museveni angali mbele Bobi Wine akisisitiza wanajeshi...

DOUGLAS MUTUA: Waandamanaji wa Amerika na wa Kenya ni...