Mshtuko wezi wakipora benki mchana

Mshtuko wezi wakipora benki mchana

Na KITAVI MUTUA

POLISI katika Kaunti ya Machakos, Jumanne walianzisha msako mkali dhidi ya majambazi watano waliovamia tawi la Equity Bank mjini Matuu na kuwapokonya bunduki polisi wawili.

Wezi hao waliokuwa wamevalia makoti makubwa na kujihami kwa bastola, yaaminika walikuwa wamejificha karibu na majengo hayo hapo awali.

Kwenye tukio hilo lililodumu karibu dakika kumi, wezi hao walivamia punde tu maafisa hao wawili waliokuwa wamejihami walipotengana na kwenda njia tofauti.

Walinda usalama hao walikuwa wameketi pamoja karibu na lango la benki hiyo lakini mara tu afisa mwanamme alipoingia katika ukumbi wa benki na kumwacha nje afisa mwenzake wa kike, alivamiwa, akatandikwa na kupokonywa bunduki yake.

Afisa huyo mwanamke alishambuliwa ghafla na majambazi watatu waliovalia makoti makubwa waliomwibia bunduki yake aina ya AK47 iliyokuwa na risasi 30.

Genge hilo liliingia benki na kumkabili afisa huyo mwingine wa polisi huku likimwelekezea bunduki na kumwamrisha ajisalimishe huku wateja wakikimbilia usalama wao.

“Mvutano ulizuka ambapo walimipiga teke kwenye nyeti zake alipozuia juhudi zao za kumpokonya bunduki,” alisema mama mboga aliyeshuhudia kisa hicho.

Walichunguza mienendo ya maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda benki hiyo, kabla ya kuwashambulia na kuwapokonya bunduki zao zilizokuwa na risasi.

Kulingana na mashahidi, namna ambavyo shambulizi hilo lilivyotekelezwa, inaashiria kuwa majambazi hao walikuwa wamechunguza matukio katika benki hiyo kwa umbali wakisubiri wakati mwafaka wa kuvamia.

Kisanga chote cha wizi huo kilichukua karibu dakika 10 huku genge hilo likitoweka kwa mguu kupitia eneo jirani la makao, likiwa na kiasi kisichojulikana cha pesa.

You can share this post!

Tutaunga Raila kwanza – Mlima

Kesi za ufisadi: Haji ajitetea