Habari Mseto

Mshukiwa alipa dhamana na kuchomoka mbio akaoe

July 31st, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

IFIKAPO Jumamosi Agosti 3 kengele za harusi zitalia ambapo mmoja wa washukiwa 12 wanaoshtakiwa pamoja na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu katika kashfa ya Sh588 milioni atafunga ndoa huku Gavana huyo akijikunyata gerezani baada ya kushindwa kupata Sh15 milioni za dhamana.

Bw Samuel Muigai Mugo atamshika mkono mpenziwe Lilian Wambui na kuapa mbele ya Kasisi wa Kanisa la PCEA kwamba “nitamtunza na kumpenda siku za maisha yangu yote hadi kifo kitutenganishe.”

Kwa Bw Muigai, kutoa kwake korokoroni ni muujiza kwa vile kiongozi wa mashtaka Vincent Monda alikuwa ameomba korti imwachilie kwa dhamana inayolingana na kiwango cha pesa kilichotoweka kutoka kwa kaunti ya Kiambu.

Lakini wakili wake Mbiyu Kamau alimtetea: “Muigai hakuchukua hata senti moja ya pesa hizo. Dhambi yake ni kwamba alikuwa mmoja wa kamati iliyotoa kandarasi hiyo. Naomba umwachilie kwa dhamana akaoe Jumamosi.”

Bw Monda alijibu na kusema, “Mshtakiwa amepanga harusi ya kukata na shoka. Kadi ya harusi ni ya thamani kuu. Mwaliko aliotoa ni kuwa maankuli yatakuwa tele na wageni wataburudika vilivyo.”

Bw Monda alimwonyesha hakimu kadi hiyo kama ushahidi. Picha/ Richard Munguti

Lakini wakili Prof Tom Ojienda alisema mshtakiwa alisaidiwa na marafiki kuandaa harusi yake.

“Mshtakiwa aliachangiwa harambee na marafiki kuandaa harusi hii itakayofungwa Agosti 3, 2019,” alisema Prof Ojienda.

Alisema makosa ya Bw Muigai na wenzake ni kutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kuidhinisha kandarasi kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited ya ujenzi wa barabara.

Mahakama ilifahamishwa kuwa makosa dhidi ya mshtakiwa huyo na wenzake wanne ni mabaya kwa vile ndiyo yalipelekea mamia ya mamilioni ya pesa kutoweka.

Alikuwa mmoja wa wale waliolipa kwanza huku Bw Waititu, aliyekuwa waziri wa ujenzi Luka Mwangi Waihinya na mwenye kampuni iliyopewa kandarasi hiyo Charles Mbuthia Chege wakishindwa kupata dhamana ya Sh15 milioni.

Mkewe Waititu , Susan Wangari, licha ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa tasilimu alishindwa kuwasilisha pasipoti yake na kulazimu azuiliwe katika gereza la wanawake la Lang’ata, Nairobi.

Akiomba apewe dhamana ndogo mBw Mugo alieleza mahakama mshahara wake ni Sh124,000 na hawezi kupata dhamana ya juu.

Ameshtakiwa pamoja na wanachama wengine wa kamati hiyo ya ukadiriaji kandarasi Zacharia Njenga Mbugua, Joyce Ngina Musyoka,Simon Kabocho Kang’ethe na Anslem Gachukia Wanjiku.

Hakimu alimwachilia Bw Muigai kwa dhamana ya Sh1 milioni pesa tasilimu ambazo alilipa upesi na kwenda kumalizia mipango ya harusi yake ya Jumamosi.