Habari Mseto

Mshukiwa aliyeingia mitini miaka 2 iliyopita anyakwa

April 17th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Mshukiwa wa ulaghai aliyetoroka miaka miwili iliyopita akikwepa kuhukumiwa hatimaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Erick Onyango Odago aliyeshtakiwa mwaka wa 2016 alichana mbuga baada ya kukiri shtaka la kughushi barua ya kampuni ya bima.

Wakili wa mshtakiwa Wambugu Wanjohi alijipata taabani alipodai mshtakiwa alikuwa mgonjwa na kulazwa hospitali kaunti ya Bungoma.

“Usijaribu kupotosha mahakama. Mshtakiwa alitoroka miaka miwili iliyopita. Alikuwa arudi kortini kuhukumiwa kisha akatoroka 2017. Mbona jamaa wake hawakufika kortini kueleza ni mgonjwa?”

Hakimu aliendelea kumweleza wakili “Mimi ni mzaliwa wa Bungoma. Nitahitaji jina la hospitali alikolazwa na jina la daktari aliyekuwa anamtibu.”

Mshtakiwa aliambia korti atabadilisha jibu la shtaka na kulikanusha lakini mahakama ikamweleza hataachiliwa kwa dhamana.

“Hiii kesi lazima iishe leo. Mshtakiwa amekuwa akisumbua polisi. Amesakwa kwa miaka miwili sasa. Shauriana naye na mtoe jawabu kwa mahakama lakini lazima hii kesi itamatishwe,” aksema hakimu.