Mshukiwa mkuu katika shambulizi la afisa wa ubalozi ndani

Mshukiwa mkuu katika shambulizi la afisa wa ubalozi ndani

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA mkuu katika kisa cha kumshambulia afisa wa Ubalozi wa Zimbabwe anayefanyakazi katika Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN) aliyekamatwa akijaribu kutorokea Tanzania amezuiliwa kwa siku 10.

Zachariah Nyaore Obadiah ameagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri hadi Machi 24, 2022 atakapofikishwa kortini pamoja na washukiwa wengine 16 waliokamatwa Jumatatu iliyopita.

Nyaore hakupinga ombi la Polisi azuiliwe kwa siku 10. “Mheshimiwa nilikamatwa na Polisi mahala pa shambulizi nikimpeleka mteja wangu Westlands.Picha yangu ilisambazwa katika vyombo vyote vya habari hadi nikaingiwa na woga na hofu kuu basi nikaamua kujificha na kutoroka,” Nyaore alimweleza hakimu mwandamizi Robinson Ondieki.

Mshukiwa huyo alieleza mahakama , hakuhusika na kisa hicho lakini hakimu akamkatiza na kumweleza “hatufanyi kesi leo. Polisi wanaomba wakuzuilie kwa siku 10 tu wakamilishe uchunguzi. Je unapinga.”

“Hapana sipingi wakinizuilia kwa siku 10. Nitamweleza afisa anayechunguza kesi hii mengi,” Nyaore aliongeza kusema. Afisa huyo wa Ubalozi wa Zimbabwe anayehudumu katika UN kitengo cha usambazaji vyakula anawakilishwa na Wakili Philip Murgor.

“Naomba hii mahakama iwaruhusu polisi kufanya uchunguzi wa kina ndipo haki itendeke na ukweli ukithiri,” Bw Murgor alimweleza hakimu.

Akiwasilisha ombi la kumzuilia mshukiwa huyo kwa siku 10, afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekta Lyvonne Mwanzia alisema Nyaore “alikamatwa akitorokea Tanzania. Alishikwa katika kituo cha mpakani cha Isebania na kusafirishwa kwa ndege hadi Nairobi.”

Insp Mwanzia alisema Nyaore ndiye mshukiwa mkuu katika kisa hicho ambapo Bi Tafadzwa Esnath Chiposi alinyang’anywa mali yake kimabavu na kudhulumiwa kijinsia. Afisa huyo alidokeza polisi wanahitaji muda kuwahoji mashahidi na kuandikisha taarifa zao kabla ya kupeleka faili hiyo afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kwa ushauri zaidi na kupewa mwelekeo.

Washukiwa wanaozuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri ni James Mutinda Muema, Samuel Wafula Muswahili, Charles Omondi Were, Japheth Bosire Obano, Hassan Farah Forah, Wanjuki Lincoln Kinyanjui, Joseph Ngugi Mbugu, Lenson Fundi Njururi , Harrison Maina Irungu, Benjamin Ngure Githimii, Ignatius Shitekha Mufwolobo,Martin Kamau Maina, Shadrack Ambia Luyeku , Shadrack Kioko Nyamai, Cliff Gikobi Oyaro and Joseph Kibui Mukambi.

Washukiwa wanane walieleza mahakama wao sio wahudumu wa boda boda.

You can share this post!

MUME KIGONGO: Kulala chini ya saa 5 kwa siku kutakugeuza...

Wazee wamfanyia kidosho tambiko kwa kutusi nyanya mkwe

T L