Habari Mseto

Mshukiwa wa mauaji ya mhadhiri azimwa kufurahia Krismasi na familia yake

December 14th, 2018 1 min read

Na JOSEPH OPENDA

MAHAKAMA KUU ya Nakuru imemzuia mshukiwa katika mauaji ya aliyekuwa mhadhiri wa lishe bora katika Taasisi ya Rift Valley ya Sayansi na Teknolojia, kufika nyumbani kwake katika msimu huu wa Krismasi.

Jaji Joel Ngugi alikataa ombi la Godffrey Kangogo lililotaka kubatilishwa kwa sheria za bondi kumruhusu kujiunga na familia yake nyumbani kwake eneo la Rongai kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya.

Bw Kangogo ambaye amekana kumuua Bi Irene Jepchumba hapo Julai 6, katika mto Molo, Kaunti Ndogo ya Rongai, alikabiliwa na sheria ngumu za korti kuhusu bondi yake.

Hata hivyo, korti ilimpa uhuru baada ya kulipa bondi ya Sh500,000 lakini ikamzuia kuenda karibu na nyumba yake.

Hii ni baada ya upande wa mashtaka kuishawihi korti kuwa mshtakiwa angevuruga ushahidi na pia kusemekana kuwatishia watu wa familia ya mwendazake ambao huishi eneo sawa.

Kupitia kwa wakili wake David Mongeri, Bw Kangogo alikuwa ameiomba korti kumruhusu kuungana na familia yake kwa burudani za Krismasi, lakini korti ikakataa.

Mwili wa Bi Jepchumba, kifungua mimba wa watoto watatu, na mwenye miaka 27 ulitolewa katika Mto Molo Julai 6. Mhadhiri huyo alitajwa na familia na marafiki kuwa mchangamfu, shupavu na mweledi.

Wanakijiji ambao waliupata mwili huo walisema ulikuwa nusu uchi. Kulingana na ripoti ya polisi, mshtakiwa alikuwa na marehemu kabla ya kifo chake.

Mshukiwa huyo alifikishwa mahakamani Julai 20, na kukanusha shtaka hilo la mauaji. Lakini familia ya mwendazake imesisitiza kuwa binti yao aliuawa kinyama.

Aidha, kusikilizwa kwa kesi hiyo kulizidi kucheleweshwa baada ya mawakili wa serikali na wale wa mshatikiwa kuendelea kuwasilisha maombi kwa mahakama ili wapewe maagizo.

Jaji Ngugi alielekeza kuwa kesi hiyo itajwe Januari 15, mwakani.