Makala

Mshukiwa wa mauaji ya Starlet Wahu aonyesha utulivu akihojiwa

January 11th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO wataendelea kumzuilia mshukiwa wa mauaji ya mwanadada Starlet Wahu kwa siku 14 zaidi ili kumaliza uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mnamo Alhamisi, Januari 11, 2024, Bw John Matara, 34, alikiri alimdunga Wahu kisu mguuni lakini si kumdunga kifuani na kichwani kama inavyodaiwa.

Wahu alikuwa ni dada mdogo wa Pasta Victor Kanyari.

Kinara wa upelelezi wa makosa ya jinai katika kaunti ndogo ya Makadara, Martin Korongo, aliambia Taifa Leo kwamba maafisa wake walikuwa na siku 21 za kumzuilia mshukiwa mkuu na kufikia Alhamisi, walikuwa na wiki mbili zinazobaki ili wamdadisi kikamilifu.

Bw Matara anazuiliwa katika seli katika kituo cha polisi cha Industrial Area kabla ya kufikishwa mahakamani mara uchunguzi wa utakapokamilika.

Marehemu Starlet Wahu. PICHA | MAKTABA

Aidha, Bw Korongo alisema anamsubiri mkuu wa polisi katika kitengo cha jinai eneo la Ruiru kumkabidhi faili nyingine ambapo Bw Matara anahusishwa na kisa kingine kuhusu mwanamke mwingine aliyeibiwa pesa kwa kutumia mabavu.

“Ninamsubiri mwenzangu kutoka kaunti ndogo ya Ruiru kuleta faili na ripoti iliyopigwa muhuri katika idara ya DCI katika eneo la Njiru ambapo mshukiwa Matara anahusishwa na uhalifu mwingine,” Bw Korongo akasema.

Aliongeza kwamba akiwa katika seli za polisi, Bw Matara huwa mtulivu sana na hapendi kuongea sana.

Alisema wakati maafisa wako na mshukiwa, huonekana mtu mtulivu, hushirikiana na maafisa hao vyema kwa kuzungumza lakini “yeye ni mtu mpole na mwenye akili nyingi.”

“Mshukiwa ni mtu anayeonekana mpole, mtulivu na akiwa ndani ya seli haongei sana. Huwa anazungumza na sisi vizuri lakini ni mtu aliye na akili nyingi kwani ni mwerevu sana,” Bw Korongo akasema.

Aliongeza kwamba katika tukio la pili, mshukiwa anahusishwa na uhalifu wa kumwibia mwanamke hela zake kupitia njia ya M-Pesa.

Alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi, ataunganisha visa vyote viwili ili afunguliwe mashtaka ya kuua na kuiba kwa kutumia mabavu.

Alisema Bw Matara amekiri kwamba alikuwa ‘ameoa’ na kujaaliwa mtoto mmoja lakini wakaachana na mke baada ya mzozo wa kinyumbani.

Mshukiwa aliangaziwa na Taifa Leo mnamo Januari 4, 2024, kufuatia mauaji ya Wahu katika chumba kimoja katika Papino Apartment eneo la South B.

Kulingana na mkuu wa Polisi katika kaunti ndogo ya Makadara, Bi Judith Nyongesa, siku ya kisanga cha South B, mwili wa Wahu ulipatikana sakafuni ukiwa katika hali mbaya na damu nyingi na alama za kudungwa mwilini zikionekana.

“Mwili ulikuwa na jeraha la kisu karibu na sikio la kushoto na pajani. Hakukuwa na majeraha mengine yaliyoonekana mwilini japo nguo za marehemu zilikuwa juu ya kochi,” Bi Nyongesa akasema.

Tukio hili liliripotiwa katika kituo cha polisi cha South B ambapo maafisa waliofika katika eneo la tukio walikumbana na mtiririko wa damu ulioashiria kutoka katika chumba cha kulala na ishara ya mapambano, kisu cha jikoni kilicholowa damu, kondomu, sindano zilizotumiwa, vifaa vya kupima maambukizi ya HIV na chupa ya mvinyo miongoni mwa bidhaa za kibinafsi.

Polisi walimsaka Bw Matara, 34, baada ya kutoroka.

Alinaswa na polisi katika kukurukakara za kupokea matibabu katika hospitali ya Mbagathi na kukamatwa pamoja na rafikiye aliyekuwa akimsaidia kupewa huduma hiyo.

Tayari majasusi wamepata nyumba alimokaa mshukiwa katika mtaa wa Kahawa West. Polisi walisema walipata kwamba katika nyumba alimoishi, kulikuwa na kitanda, nguo na kiti kimoja.

Vilevile, Bw Korongo ameongeza kwamba maafisa wa upelelezi wana ripoti nyingine kuhusu matukio mengine ya uhalifu katika eneo la Ngong na Kasarani yanayomlenga Bw Matara kama mshukiwa.