Habari Mseto

Mshukiwa wa mauaji ya Wakili Kimani hakuwa mgonjwa – Daktari

February 20th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI wa Idara ya Magereza Joseph Wambugu Jumanne alieleza Mahakama Kuu Kachero Peter Ngugi Kamau alipelekwa katika gereza la Naivasha kutibiwa maumivu yasiyomo.

“Nilimkagua na kumpima Ngugi na sikumpata na ugonjwa wowote,” Dkt Wambugu alimweleza Jaji Jessie Lesiit.

Daktari huyo alisema alipomkagua Ngugi hakuona akiwa na majeraha yoyote mwilini mwake.

Mahakama ilifahamishwa kile mshtakiwa alipewa ni tembe za kutuliza maumivu kama vile kichwa ama uchovu.

“Mshtakiwa alikuwa buheri wa afya na kamwe sikumwona na majeraha mwilini,” Jaji Lesiit alielezwa.

Daktari huyo wa Serikali alisema hayo alipotoa ushahidi katika kesi ambapo Ngugi na maafisa wanne wa polisi wa utawala kutoka kituo cha Syokimau wameshtakiwa kuwaua wakili Willy Kimani , mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri mnamo Juni 23, 2016.

Mahakama ilifahamishwa na daktari huyo alikuwa ameagizwa ampime mshtakiwa huyo majeraha ya mwili mnamo Septemba 2016.

Shahidi huyo alisumulia hayo katika kesi inayowakabili Ngugi, Fredrick ole Leliman, Stephen Cheburet, Bi Sylvia Wanjiku na Leonard Maina Mwangi kwa mauaji ya Kimani, Mwenda na Muiruri mnamo Juni 23, 2016.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao Cliff Ombeta na Nelius Mucera Kinyori wamepinga maungamo ya Ngugi mbeke ya Inspekta Mkuu Geoffrey Waruru Kinyua kwamba watano hao ndio waliohusika na mauani ya kinyama ya Kimani, Mwenda na Muiruri.

Jaji Lesiit aliamuru mashahidi wote walioshuhudia maungano hayo wafike kortini kwanza waeleze jinsi mambo yalivyokuwa ndipo korti iamue ikiwa itapokea ushahidi huo wa kurasa 21 au la.

Insp Kinyua alieleza mahakama alirekodi ushahidi wa Ngugi katika makao makuu ya uchunguzi wa jinai (DCI) baada ya kupelekwa na Insp Clement Mwangi, ambaye ni afisa mkuu anayechunguza kesi hiyo.

Kachero Ngugi alikuwa ameandamana na ndugu yake alipoandikisha taarifa hiyo ya maungano jinsi wahasiriwa walivyotekwa nyara, kuzuiliwa katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau kabla ya kutolewa usiku na kuuawa katika shamba lililowazi Mlolongo.