Habari Mseto

Mshukiwa wa sakata ya Kimwarer na Arror abambwa JKIA

December 23rd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAPELELEZI kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walimkamata Mkurugenzi wa Ukusanyaji Rasilimali katika Hazina ya Kitaifa Jackson Kinyanjui katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jumapili usiku.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa katika akaunti ya Twitter ya DCI, Bw Kinyanjui ni mmoja wa washukiwa wakuu katika sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror ambapo inashukiwa kuwa Sh21 bilioni zilipotea.

Mshukiwa huyo alikamatwa dakika chache baada ya ndege iliyombeba kutua katika uwanja wa JKIA Jumapili usiku kutoka Amerika.

Ilani ya kukamatwa kwa Bw Kinyanjui ilikuwa imetolewa na DCI mmnamo Julai 22, 2019.

“Jackson Njau Kinyanjui, mshukiwa anayesakwa alikamatwa Jumapili usiku alipowasili kutoka Amerika kufutia amri iliyotolewa na makao makuu ya DCI Julai 22, 2019.

“Mshukiwa ambaye anatakikana kuhusiana na kosa la ulaghai katika sakata ya Arror na Kimwarer alisimamisha na maafisa wa idara ya uhamiaji kabla ya kuwasilishwa kwa wapelelezi wa DCI,” ujumbe huo ukasoma.

Mnamo Julai mwaka huu, Waziri wa Fedha aliyesimamishwa kazi Henry Rotich na aliyekuwa Katibu katika Wizara hiyo ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali waliokamatwa kuhusiana na sakata hiyo.

Wengine waliokamatwa ni pamoja na aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ustawi wa Kimaeneo Susan Koech, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawi wa Bonde la Kerio (KVDA) Kipchumba Kimosop na Afisa wa Masuala ya Kiuchumi katika Wizara ya Fedha Kennedy Nyachiro.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) Geoffrey Wahungu pia alikamatwa nyumbani kwake katika eneo la Rukundi, kaunti ya Tharaka Nithi.

Walishtakiwa mahakama na mpaka sasa kesi zao hazijamalizika.