Habari za Kitaifa

Mshukiwa wa ujambazi asimulia walivyoua wanawake alipokuwa genge la Confirm Nakuru

April 17th, 2024 2 min read

Na JOSEPH OPENDA

MAKOSA ya mshukiwa mkuu katika mauaji ya kinyama ya wanawake katika eneo la Mawanga, Kaunti ya Nakuru, yaliyotekelezwa 2021/2022, yalisababisha genge lote lililohusika kukamatwa.

Maelezo mapya yaliyowasilishwa mbele ya Mahakama ya Nakuru yamefichua jinsi Evans Michori Kebwaro, anayedaiwa kupanga mauaji hayo, alivyoishia kutumia simu iliyoibwa kutoka kwa mmoja wa wahasiriwa na kutumbukiza genge lote mashakani.

Ushahidi mpya aliokiri Michori Aprili 15, 2024 na uliorekodiwa katika maafikiano kati ya upande wa mashtaka na mlalamishi, unafichua jinsi mshtakiwa na washirika wake, baada ya kukaa mafichoni kufuatia ripoti za vyombo vya habari kuhusu maovu yao, alivyoshawishika kutumia simu iliyoibwa kutoka kwa mwathiriwa, Beatrice Akinyi Adhiambo, ambaye mauaji yake yalikuwa yangali yanachunguzwa na polisi.

Michori aliweka kadi yake binafsi ya simu katika simu hiyo na kutuma ishara kwa polisi kwa kuwa nambari maalum ya simu, IMEI, ilikuwa imeripotiwa kuibiwa katika kisa kingine eneo la Mawanga.

Polisi walifuatilia ishara hiyo hadi nyumbani kijijini kwa Michori, eneo la Masimba, Kaunti ya Kisii ambapo alikamatwa na washirika wake watano Kevin Omondi, Josephat Simiyu, Julius Omondi, Isaac Kinyanjui, na Dennis Alusiola kutambuliwa.

Washukiwa hao sita ambao ni wanachama wa genge sugu la Confirm lililopigwa marufuku Nakuru walikamatwa na kushtakiwa kwa kesi kadhaa za mauaji.

Walishtakiwa kwa mauaji ya wanawake wanne wakiwemo Beatrice Akinyi, Grace Wanjiku, Diana Opicho na Susan Wambui waliouawa tarehe tofauti kati ya Disemba 21, 2021 na Juni 24, 2022.

Katika muafaka na korti, Michori alikiri kutekeleza mauaji hayo bila kukusudia na kutoa maelezo ya kina kuhusu shughuli za genge hilo.

Alikiri jinsi alivyopanga kwa makini na kutekeleza shambulizi na mauaji ya Grace Wanjiku Kariuki, chini ya uongozi wa Kevin Omondi na vitendo vya kinyama vya genge hilo.

Kulingana na Michori, genge hilo la majambazi sita lilikutana saa tatu asubuhi katika uwanja wa Kanisa la Kingdom Seekers ili kupanga maovu yao.

Baadaye waliondoka kwa pikipiki kuelekea nyumbani kwa mwathiriwa eneo la Mawanga wakiongozwa na Kevin Omondi.

Walijitambulisha kama maseremala

Stakabadhi ya korti inasema Kevin aliwaagiza Simiyu na Kinyanjui kwenda katika duka lililokuwa karibu na barabara na kuzungumza na Grace, aliyekuwa akiendesha duka hilo la familia mama yake alipokwenda kanisani.

“Simiyu na Kinyanjui walijitambulisha kwa mwanamke huyo kama maseremala waliotumwa na mama yake kufanyia ukarabati samani nyumbani kwao. Mwanamke huyo aliwapuuza baada ya kuthibitisha na mama yake kwamba hakuwa ametuma mtu yeyote kufanya kazi kama hiyo,” anasema Bw Michori.

Hata hivyo, wanaume hao waliingia dukani na kumkamata Wanjiku alipokuwa akiwasiliana na mama yake kupitia simu, na kuwaruhusu majambazi waliosalia kuingia.

“Kevin alimwekelea Grace kisu shingoni na kumwelekeza nyumba kuu. Kevin na Dennis walimpeleka chumbani na kumuua. Dennis alikuja na kutuagiza tukiwa na Julius twende kutazama ikiwa kulikuwa na pesa dukani,” alisema Michori.

Walipata Sh2,500 ambazo walichukua pamoja na kadi za benki kabla ya kurejea na kumpata Kinyanjui akipakia TV ya inchi 32 ndani ya boksi.

Walipokuwa wakijiandaa kuondoka, Michori alisimulia jinsi Kevin alimwagilia nyumba hiyo petroli na kuiwasha moto kabla ya wauaji hao kutoroka kwa kutumia pikipiki.

Mama yake Wanjiku alijulishwa kuhusu moto huo ambapo alikimbia nyumbani na kuwapata majirani wakijaribu kuuzima.

Mwili wa binti yake ulipatikana ukiwa umelazwa kitandani na kuteketezwa kabisa bila ishara za kung’ang’ana kujaribu kutoroka moto.

Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kiugoini, eneobunge la Bahati.

Genge hilo lilikutana jioni katika eneo lao la mkutano katika Kanisa la Kingdom Seekers ambapo Michori alipatiwa na Kevin Sh2,000.

Unyama wa genge hilo ulifichuliwa zaidi na ripoti ya upasuaji Juni 23, 2022, iliyofichua dalili za kunyongwa na majeraha kwenye sehemu nyeti za mwili wa Wanjiku.

Michori tayari amekiri kuhusika katika mauaji ya mwanamke mwingine.