Mshukiwa wa ulaghai wa mamilioni azuiwa kusafiri

Mshukiwa wa ulaghai wa mamilioni azuiwa kusafiri

Na RICHARD MUNGUTI

IDARA ya Uhamiaji Jumanne iliamriwa imzuie David Kahi Ambuku kusafiri, mshukiwa aliyetoroka kesi ya upokeaji zaidi ya Sh14milioni katika kashfa ya uuzaji bidhaa katika Idara ya Ulinzi.

Na wakati huo huo Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai alipewa muda wa mwezi mmoja kumtia nguvuni Bw Ambuku na kumfikisha kortini.

Bw Ambuku anayeshtakiwa pamoja na washtakiwa wengine wanane, alitoroka punde tu alipoachiliwa kwa dhamana.

Wengine alioshtakiwa nao ni Clifford Okoth Onungo almaarufu Victor Wandera, Samuel Murumet Maasai, Dedan Waithaka Mwangi, Elysha Onyango Oswago, Cliff Moseti Obwogi, Esther Kalungo Ngotho, Boniface Kamau Macharia na Allan Kiprotich Chesang.

Pia hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku aliamuru mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai (DCI) ateue maafisa zaidi kumwandama Ambuku.

Afisa anayechunguza kesi hiyo alieleza mahakama kuwa amekuwa akimsaka Ambuka pasi mafanikio.

“Taarifa simu yake iliyotayarishwa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom yaonyesha kuwa mshtakiwa amekuwa akisafiri kati ya Nairobi na Kampala,” hakimu alielezwa.

Bi Mutuku alifahamishwa kwamba Ambuka amekuwa akidai ni mgonjwa lakini rekodi yaonyesha aliondoka hospitali kitambo.

Bi Mutuku alisema kesi hiyo haijawahi sikizwa licha ya kuwasilishwa kortini kwa siku nyingi.

“Baadhi ya washtakiwa katika kesi hii hawajajibu mashtaka licha ya kuachiliwa kwa dhamana,” alisema Bi Mutuku.

Bi Mutuku alimtaja Bw Boniface Kamau Macharia kuwa miongoni mwa washtakiwa ambao hawajasomewa mashtaka na kuyajibu.

Hakimu alimwamuru DCI aongeze idadi ya maafisa wanaomwandama Ambuka na “akifikishwa kortini hatua ifaayo itachukuliwa.”

Mahakama ilifahamishwa kiwango cha dhamana cha Sh300,000 walichopewa washtakiwa ni kidogo mno. Lakini hakimu akamweleza mshtakiwa

kiwango cha dhamana hakina uhusiano na mshtakiwa kutoroka. Mahakama iliamuru kesi hiyo itajwe Machi 8,2021.

Washtakiwa Clifford Okoth Onungo almaarufu Victor Wandera, Samuel Murumet Maasai, Dedan Waithaka Mwangi, Ambuku Elysha Onyango Oswago, Cliff Moseti Obwogi, Esther Kalungo Ngotho, Boniface Kamau Macharia na Allan Kiprotich Chesang wanakabiliwa na mashtaka mbali mbali ya kughushi zabuni za kuuzia idara ya ulinzi (DoD) bidhaa.

Wote wanakabiliwa na shtaka la kughushi barua ya kuwakubalia watekeleze ujenzi katika idara ya DoD kupitia kwa kampuni ya WIL Developers and Construction Limited.

Wote tisa wamekanusha shtaka la kughushi barua ya kandarasi hiyo inayodaiwa ilikuwa imetiwa sahihi na katibu mkuu idara ya ulinzi Bw Torome Saitoti na afisa mkuu kitengo cha fedha Bw Rotich K.

Tena washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kughushi arifa ya kisiri ya zabuni hizo ya Januari 18 2018 ya kununulia DoD Magunia ya Nailoni ya uzani wa kilo 50 iliyokuwa imekabidhiwa mkurugenzi wa WIL Developers and Construction Limited.

Shtaka la nane dhidi yao lasema kuwa mnamo Feburuari 1 2018 katika benki ya Standard Chartered walipokea kwa njia ya undanganyifu Sh14m kutoka kwa Bw Johnson Mwanzia Wambua wakidai walikuwa wamepewa kandarasi ya kununulia DoD magunia.

You can share this post!

Red Star Belgrade anayochezea Mkenya Richard Odada kualika...

Ndani miaka 10 kwa kumuumiza mpenziwe