Habari Mseto

Mshukiwa wa wizi wa mamilioni atokwa na jasho ajabu kizimbani

May 26th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI  wa kampuni mbili anayekabiliwa na shtaka la wizi wa Sh76 milioni aliamriwa apelekwe hospitali baada ya kuugua akiwa kizimbani kabla ya kusomewa mashtaka.

Bw Samson Njenga Waweru (pichani) mwenye umri wa miaka 38 alianza kutoka na jasho na kutetemeka akiwa kizimbani akisubiri kesi inayomkabili iitwe.

Bw Waweru ambaye ni mkiurugenzi wa kampuni mawili za Unified Concepts Limited na Hosted Farms Limited alianza kutetemeka na kububujikwa na jasho.

Mshtakiwa aliletewa chupa ya lita moja ya maji ya Dasani kutuliza joto lakini hakusaidika.

Alipoitwa kufika mbele ya hakimu mkazi Bi Mirriam Mugure hakuweza kusimama kwa sababu ya kutetemeka.

Nguo zake zililowa jasho ndipo akamtazama na kuamuru , “Mshtakiwa anaonekana ni mgonjwa. Anatokwa na jasho jingi. Hawezi kusomewa mashtaka jinsi alivyo.”

Bi Mugure alisema sheria imesema mshtakiwa asomewe mashtaka ama kufanya kesi  akiwa buheri wa afya.

Hakimu aliamuru polisi wampeleke hospitali ya Kenyatta mara moja kisha ripioti ya daktari iwasilishwe kortini Mei 29, 2018.

Bw Waweru anakabiliwa na shtaka la kuiba Sh76 milioni mali ya Dufry Kenya Limited kati ya  Desemba 19, 2016 na Septemba 12, 2017.

Mkurugenzi huyo hakusomewa mashtaka manne kwa vile alikuwa mgonjwa.