Habari Mseto

Mshukiwa wa wizi wa zulia auawa Zimmerman

March 24th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MSHUKIWA wa uhalifu eneo la Zimmerman aliuawa kinyama Jumatatu katika kisa ambapo inadaiwa alitandikwa na kundi la walinzi binafsi waliomfumania akitekeleza wizi.

Mwanamume huyo na ambaye majina yake halisi hayakufahamika, inadaiwa alipatikana akiiba zulia katika ploti moja ya watu kuishi kwa kulipia kodi.

Kulingana na waliomjua, inadaiwa si mara yake ya kwanza kushiriki visa vya wizi na uhalifu mitaa mbalimbali Nairobi.

“Hukamatwa, anashtakiwa kortini. Akimaliza kuhudumu kifungo cha jela anarejea kutekeleza uhalifu,” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka atajwe.

Mwili wake ulionekana kuwa na majeraha mabaya kichwani, kwenye kifua na mikono, jambo linaloashiria alifuja damu ndani kwa ndani kupita kiasi.

Walioshuhudia kisa hicho wanadai alikawia kwa muda wa saa kadhaa akichechemea kwa maumivu, kabla kuaga dunia.

“Nilipotaka kumpa maji niolionywa kuwa ni hatari, yangesababisha kifo,” akasimulia mama mmoja na aliyeomba jina lake lisichapishwe.

Licha ya kupekuliwa na maafisa wa polisi, hakuna stakabadhi zozote kama vile kitambulisho au simu, zilizopatikana.

Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

Visa vya uhalifu na wizi wa nguvu za kimabavu eneo la Zimmerman vinaendelea kuongezeka, wenyeji wakiomba idara ya usalama kuimarisha ushikaji doria.