Mshukiwa wa wizi wa vyuma vilivyoibwa kutoka Industrial Area akamatwa Kayole

Mshukiwa wa wizi wa vyuma vilivyoibwa kutoka Industrial Area akamatwa Kayole

NA SAMMY KIMATU

MAAFISA wa polisi kutoka Makadara wamemkamata mshukiwa mmoja na kupata bidhaa kadhaa ambazo ripoti za polisi zilionyesha ziliibwa katika bohari moja katika eneo la Viwanda, kaunti ya Nairobi.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo ameambia Taifa Leo kwamba hatua hiyo inajiri siku moja tu baada ya wahalifu waliokuwa wamejihami kuvamia kampuni ya ujenzi katika eneo lililoko karibu na barabara ya Shimo La Tewa.

Wakati wa uvamizi huo, wahalifu hao waliwavamia walinzi wawili waliokuwa wakilinda eneo la ujenzi kabla ya kuwafunga mikono, miguu na kuwafumba midomo.

Shehena ya vifaa kutoka eneo hilo iliporwa kabla ya washukiwa hao kuliondoa gari hilo kwa kutumia lori.

Hata hivyo, kutokana na mazingira ambayo walinzi walikuwa nayo, hawakuweza kurekodi namba za usajili za gari hilo.

Bw Odingo aliongeza kuwa walinzi hao wawili walitupwa kwenye ghorofa ya chini ya jengo hilo na kuachwa wakidhaniwa wamekufa.

“Washukiwa hao ambao idadi yao haijafahamika waliiba vifaa vya aina tofauti vya ujenzi pamoja na mashine kwenye eneo la ujenzi. Pia waliwatupa walinzi wawili katika sehemu ya chini ya jengo hilo kabla ya kutoroka na mali,” Bw Odingo aliambia Taifa Leo.

Ingawa hivyo, kisa hicho kimechukua mkondo mwingine baada ya dereva wa lori kuwaambia maafisa wa polisi kuhusu tukio hilo.

Dereva amekiri kisa hicho kilimweka “baridi” lakini  ‘aliguswa’ baada ya kumuona mlinzi mmoja amefungwa kwenye kona ya orofa katika eneo lenye giza kidogo.

“Nilitii nikiwa chini ya amri kali ya wahalifu ‘kushirikiana’ na kuonywa kutoleta kile walikiita ni ‘mbinu chafu’ wakati wa kazi niliyoajiriwa kufanya,” anakumbuka.

Dereva ambaye polisi walisema alijitambulisha kama Bw Ismael Kibet Rotich, dereva wa KCG 233Y Isuzu FRR aliongeza kuwa aliajiriwa kusafirisha vifaa vya ujenzi kutoka barabara ya Shimo La Tewa katika Eneo la Viwanda hadi Kayole.

Bw Rotich anasema aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Makongeni na kuongeza kwamba alishuku vifaa hivyo vilikuwa mali ya wizi kwani alipoondoka kwenye eneo la ujenzi, alikuwa akiharakishwa kuondoka eneo la tukio na kuamriwa aendeshe gari hilo kwa mwendo wa kasi.

“Niliharakishwa na kuagizwa kuendesha gari kwa kasi lakini wakati nikitoa gari nje, niliona mtu akiwa amefungwa kamba jambo ambalo lilinisumbua na kuona sio mpango mzuri na kuamua kuripoti suala hilo kwa askari wa kituo cha polisi cha Makongeni,” Bw Rotich alisema.

Bw Odingo ameambia Taifa Leo kuwa askari wake wanaovalia kiraia waliungana na Bw Rotich hadi Kayole ambako alishusha vifaa na mashine zilizoibwa katika eneo lililotelekezwa.

Maafisa hao walifanikiwa kumkamata mshukiwa James Juma mwenye umri wa miaka 29, mkazi wa Mukuru-Kwa-Reuben katika kaunti ndogo ya Embakasi Kusini.

Kamanda wa polisi ameongeza kuwa askari hao walifanikiwa kupata vyuma vya ujenzi aina ya  D10 -15 na D12 -168, Sepeto, Ekseli 2, mashine 5, mashine 2 za kuchomelea, mfuko mweusi uliokuwa na buti, paipu ya maji na nyundo.

Baadaye walipeleka vifaa hivyo katika kituo cha polisi cha Makongeni huku mshukiwa akiwa chini ya ulinzi wa polisi nao msako mkali wa kuwakamata washirika wake mshukiwa ukianzishwa.

“Nina imani na nina hakika kwamba tutawakamata wenzake kwa sababu makachero wanaendelea vyema na uchunguzi wao. Huu ulikuwa uhalifu uliopangwa awali na vizuri na unahusisha watu wengine kadhaa. Mkono mrefu wa sheria utawanasa,” Bw Odingo alifoka.

skimatu@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Uhispania wakomoa Ureno ugenini na kutinga nusu-fainali za...

Ziwa Naivasha hatarini

T L