Bambika

Msiba wa mwana wamleta hadharani ‘mpoa’ wa KarehB

April 22nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

AJALI ya barabarani iliyosababisha kifo cha Joseph Mwadulo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika shule ya upili ya Chavakali, ilimleta hadharani babake mzazi Bw Morrison Mwaghogho.

Wengi walijua mamake Mwadulo ambaye ni mwanamuziki Mary Wangare Gioche almaarufu KarehB lakini hawakumfahamu Bw Mwaghogho.

KarehB ni mzawa wa Kaunti ya Murang’a na ambaye anafahamika vyema katika safu ya usanii ambapo amerekodi ngoma kadha, zingine zikiwa ni kwa ushirika na msanii wa mtindo wa Mugithi ambaye ni Jose Gatutura.

Mwanamuziki Mary Wangare Gioche almaarufu KarehB akiwa na msanii wa mtindo wa Mugithi ambaye ni Jose Gatutura. PICHA | MAKTABA

Uvumi umekuwa mwingi ambapo katika mitandao ya kijamii wengi wamekuwa wakiwadhania wawili hao kuwa na uchumba.

Hali haijakuwa ikisaidiwa na ucheshi wa KarehB mitandaoni ambapo amekuwa akisema kwamba “Gatutura ni rafiki wangu ambapo mimi huenda kwake kula chakula cha jioni na pia yeye huja kwangu na tunakula chakula cha jioni”.

Hata hivyo, baada ya ajali hiyo ya Aprili 1, 2024 iliyohusisha basi la Easy Coach lililoanguka katika mzunguko wa Mamboleo Kaunti ya Kisumu, imesaidia kumleta hadharani Bw Mwaghogho ambaye pia hutumia jina Mwadulo kama la kikazi.

“Kwa utamaduni wetu wa majina babangu ndiye alikuwa akiitwa Mwadulo huku nami nikiwa na jina Mwaghogho. Lakini kitaaluma nikachukua jina Mwadulo kama langu na ambalo liliishia pia kuwa la mwanangu wa kiume ambaye ni Joseph Mwadulo,” akasema.

Hali hiyo aliiweka wazi katika misa ya wafu iliyoandaliwa katika kanisa la the Christ Is The Answer Ministries (CITAM) katika mtaa wa Karen na pia katika mazishi ya mwendazake yaliyoandaliwa katika Kaunti ya Embu mnamo Aprili 12, 2024.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Mwaghogho alisema “sina mengi ya kusema ila tu nimempoteza rafiki na mwandani wangu”.

Lakini alikubali tu kwa kuwa ni hiari ya Mungu.

Alisema kwamba yeye amekuwa akichapa kazi kama mwelekezi wa vipindi, mbunifu wa michezo ya uigizaji na kwa ujumla uandishi wa nakala za uigizaji.

“Mimi ndiye nilikuwa nikiandika nakala za vipindi maarufu kama Inspekta Mwala, Tahidi High, Machachari, Mother In Law na Makutano Junction,” akasema.

Alimpata mwendazake kama kifungua mimba miaka 17 iliyopita.

“Safari yangu na mtoto huyo imekuwa ya kufana na nilifurahia hata ubunifu wake wa lugha ambapo alipenda sana kunisanifisha lugha yangu ya Kiingereza kwa matamshi na maandishi,” akafichua.

Bw Mwaghogho alisema kwamba kwa sasa atajituma kukubali mapenzi ya Mungu “ambaye kwa mapenzi yake alinijalia mtoto huyo kwa miaka 17 na kwa sasa akaonelea tu amuite aende akapumzike mbinguni”.

Bw Mwaghogho alisema kwamba “nimefurahishwa na mapenzi ambayo watu wamenionyesha na pia risala za rambirambi za kutupa moyo kutoka kwa mashabiki wetu kama familia ya usanii”.

Mtu wa maneno machache na umakinifu wa kimaongezi, Bw Mwaghogho amesema kwamba “wingu hili la simanzi limenifedhehesha lakini litaondoka kwa maisha yangu kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hatimaye atujalie neema zake”.

[email protected]