Habari Mseto

Msichana achomwa na mama mzazi kwa kuchelewesha nyanya

June 19th, 2019 2 min read

Na SAMMY KIMATU

MSICHANA wa kidato cha pili anauguza majeraha ya moto mwilini baada ya mamaye kudaiwa kumchoma alipokawia kuleta nyanya za kukaangia mboga baada ya kutumwa kibandani mtaani mmoja wa mabanda katika Kaunti ya Nairobi.

Kisanga hicho kilitokea katika Eneo la Mangala, mtaani wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba katika wadi ya Landi Mawe, ilioko kwenye eneobunge la Starehe.

Fauka ya kisanga hicho kufanyika mwishoni mwa wiki, kilifichwa polisi lakini wasamaria wema wakaamua kuwaambia wahudumu wa afya na masuala ya watoto mtaani huo ili muathiriwa apate usaidizi.

Binti huyo ana umri wa miaka 16 na anadaiwa kushambuliwa kwa stovu iliyokuwa ikiwaka moto na mama yake aliyetambuliwa na polisi kama Bi Irene Adhiambo.

Ana majeraha ya kuchomeka mgongoni, mkono wake wa kulia sawia na kwenye kiuno chake.

Kulingana na mhudumu wa masuala ya watoto eneo hilo, Bi Jane Peter, alipoarifika aliwasili nyumbani kwa mwathiriwa na akisaidiana na wenzake  wakamkimbiza Lengo Medical Clinic (LMC) kutibiwa.

Mkurugenzi mkuu wa LMC, Dkt Kennedy Kipchumba alisema mwathiriwa alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Msichana huyu alikuwa kidato cha upili katika shule moja kwenye wodi ya Nairobi South Kabla ya kuhamia katika shule nyingine ya upili ilioko mtaani humo,” Bi Jane akaeleza.

Akiongea na Taifa Leo Dijitali, dada mkubwa wa mwathiriwa, Florence Atieno alisema dadaye alitumwa nyanya na mamake mwendo wa saa moja za usiku lakini akarudi baadaye mwendo wa saa tatu za usiku.

“Ndio dadangu mdogo alitumwa na mamangu kununua nyanya lakini alirudi mweno wa saa tatu za usiku licha ya kutumwa mwendo wa saa moja,” Bi Atieno akasema.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Jacob Ibrahim alikashifu kitendo hicho na kuwashauri dada watatu tuliopata ndani ya nyumba hiyo kwamba ni lazima watoto wawatii wazazi wao.

“Nawashauri msome kwa bidii na msimchukie mama yenu kwa sababu bado ndiye mama yenu na anawasomesha,’ Bw Jacob akanena.

Bi Jane alieleza kwamba aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Industrial Area- OB No/22/14/06/2019.

Hata hivyo, mamake msichana amechana bunga na polisi wameanzisha msako mkali wa kumkamata.

Taifa Leo Dijitali ikichapisha habari hii, mama huyo anayeaminika kufanya kazi katikati ya jiji la Nairobi hakuwa ametiwa baroni.