Kimataifa

Msichana aliyecharaza wanajeshi wa Israeli makofi aachiliwa

July 30th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

Msichana wa Kipalestina aliyefungwa jela kwa kuwachapa makofi wanajeshi wa Israeli, aliachiliwa huru jana baada ya miezi minane gerezani.

Ahed Tamini alinaswa kwenye video iliyosambazwa kote ulimwenguni akiwachapa wanajeshi hao kwa kuwadhulumu wapalestina.

Tamimi, 17, na mama yake Nariman waliondolewa kwa gari kutoka gereza la Sharon hadi West Bank, wanakoishi, msemaji wa gereza Assaf Librati alisema.

Assaf alisema walikabidhiwa wanajeshi wa Israel, ambao waliwapeleka hadi kijiji chao cha Nabi Saleh.

Baada ya kuachiliwa na wanajeshi hao, Tamimi alitoa hotuba fupi kwa umati na wanahabari waliokusanyika akisema alitarajia kuhutubia mkutano mkubwa wa wanahabari baadaye.

Kulizuka taharuki kabla ya Tamimi kuwasili huku wanaume wachache waliokuwa na bendera za Israeli wakiwakaribia wafuasi waliokuwa na bendera za Palestina.

Walirushiana maneno lakini ghasia hazikutokea.