Habari Mseto

Msichana amchoma kisu mpenziwe

October 1st, 2020 1 min read

NA FAUTINE NGILA

Polisi Jumatano walimkamata msichana wa Darasa la Sita baada ya kumdunga mpenziwe wa kidato cha pili Nairobi maeneo ya Lang’ata.

Kisa hicho kiliwaacha wakazi na mshangao mkubwa. Kulingana na  shahidi aliyezungumza na polisi, wawili hao walikuwa na mzozo kabla ya msichana huyo kumdunga mwenzake kisu kifuani.

Majirani walisema kwamba walisikia duru na kuitikia wito huo na ndipo walipata mvulana akiwa amelowa damu huku akiwa na maumivu makali.

Kulingana na jirani mmoja, wawili hao walianza kuzozana baada ya mshichana huyo kumlaumu mvulana huyo kwa kuzungumza na msichaana mwingine.

“Walipokuwa wakizozana msichana huyo alichukua kisu akamdunga mwezake kifuani mara mbili,” walisema majirani.

Hapo  ndipo kijana huyo wa miaka 19 alikimbizwa hospitali ya St Mary lakini akathibitishwa kufariki walipowasili. Mwili wake ulipelekwa kwenye hifadhi ya  maiti ya City.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Lang’ata  Gregory Mutiso alithibitisha kisa hicho huku akisema kwamba mshukiwa anazuiliwa kwenye kutuo cha polisi cha Lang’ata.

“Tunamzuilia mshukiwa kwa mazungumzo zaidi kabla ya kushtakiwa,” alisema.

Mama wa msichana huyo wa miaka 15 alisema kwamba hakuwa na habari mahala mwanawe alikuwa wakati wa tukio hilo.