Habari Mseto

Msichana amuua mwanamume aliyemtongoza

December 11th, 2019 1 min read

VITALIS KIMUTAI na DICKENS WASONGA

MWANAFUNZI wa kike wa kidato cha pili alimuua mwanamume kwa kumdunga kisu baada ya mzozo kuzuka baina yao katika soko lililoko Boito, Kaunti ya Bomet Jumatatu usiku.

Walioshuhudia kisa hicho walisema mwanamume huyo ambaye hufanya kazi ya kupiga viatu rangi alikuwa akijaribu kumtongoza msichana huyo wa shule.

“Inadaiwa kuwa mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 29 alijaribu kumtongoza msichana huyo. Mwanafunzi huyo alipokataa walianza kuzozana,” akadai chifu wa kata hiyo John Cheruiyot.

Kulingana na ripoti ya polisi, mauaji hayo yalitokea mwendo wa saa tatu na nusu za usiku.

“Mshukiwa alikamatwa na kisu alichotumia kutekeleza uhalifu huo katika eneo la tukio kikiwa na madoa ya damu,” akasema kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Konoin Alex Shikondi katika taarifa.

Alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Mogogosiek akisubiri kushtakiwa. Mwili wa mwendazake umehifadhiwa katika hifadhi ya Hospitali ya Kapkatet iliyoko kaunti jirani ya Kericho kusubiri kufanyiwa upasuaji.

Mauaji mengine

Kwingineko, msichana mwenye umri wa miaka 15 Jumatatu jioni alidungwa kisu na mvulana mpenzi wake katika kijiji cha Awilo, eneobunge la Gem, kaunti ya Siaya.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Gem Bi Harriet Kinyua aliambia Taifa Leo kwamba msichana huyo aliyetambuliwa kama Maragret Auma Magga alidungwa kisu shingoni mwendo wa saa tisa za mchana na kufariki papo hapo.

Bi Kinyua alisema msichana huyo alidungwa kisu na mpenziwe baada ya mahusiano yao kuvunjika.

Kulingana na afisa huyo, mshukiwa amewahi kushtakiwa kwa kosa la unajisi na kesi yake ingali katika mahakama moja mjini Siaya.

Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Yala Level 4 kusubiri kufanyiwa upasuaji.

Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 23 aliyetambuliwa kama Fredrick Akula Onyango alikamatwa baadaye katika kijiji cha Kadhasi ‘A’ kilichoko katika kata ndogo ya Wagai Magharibi na anawasaidia polisi katika uchunguzi.