Habari za Kitaifa

Msichana atembea 15km kujiunga na shule akiwa hana hata senti

January 15th, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 kutoka eneo la Butere amewashangaza wengi baada ya kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 15 hadi Mumias akitamani kujiunga na Shule ya Upili ya St Mary’s Girls.

Diana Nyarotso akiwa amevalia sare ya samawati aliyokuwa akitumia katika Shule ya Msingi ya Ebulafu alibeba bahasha iliyosheheni barua yake ya kuitwa kujiunga na Shule ya Upili ya St Mary’s na nakala ya matokeo yake kwenye mtihani wa KCPE.

Viatu vyeusi alivyokuwa amevalia vilikuwa vimejaa vumbi na kugeuka rangi ya hudhurungi ishara ya mwendo aliokuwa ametembea hadi kufika kituo alichokusudia.

“Nilisomea katika Shule ya Msingi ya Ebulafu ambapo nilipata alama 375 katika mtihani wangu wa KCPE na kuitwa Shule ya Upili ya St Mary’s,” alieleza.

“Lakini baba yangu aliaga dunia 2012 naye mama yangu anaugua hawezi kumudu kunilipia karo ya shule. Ndiyo sababu nilirauka alfajiri na nikaanza kutembea ili nije kumsihi mwalimu mkuu wa St Mary’s akubali nijiunge na Kidato cha Kwanza. Nimejitolea kusoma na kuwa wakili ili niwasaidie wasiojiweza katika jamii.”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya St Mary’s Monicah Buchichi alisema alipigwa na butwaa wakati msichana huyo alipomwendea bila chochote akitaka kujiunga na shule hiyo.

“Nilipomhoji zaidi, niligundua kuwa anatoka familia maskini na hali yake ikanigusa. Sina hiari ila kumruhusu kujiunga na kusaka raslimali za kumwezesha kupata mahitaji yote anayohitaji shuleni,” alisema Bi Buchichi.