Lugha, Fasihi na Elimu

Msichana skauti wa Gredi ya Tatu ashiba sifa kwa kung’ara Madaraka Dei

June 5th, 2024 1 min read

NA JESSE CHENGE

MWANAFUNZI msichana jasiri wa Gredi ya Tatu aliyesisimua wakati wa gwaride la maskauti ambapo walimtumbuiza Rais William Ruto katika uwanja wa Masinde Muliro-Kanduyi, anaendelea kutunukwa sifa kote nchini.

Joy Baraka kutoka Shule ya Msingi ya Bungoma DEB, alipita uwanjani kwa ukakamavu wakati wa sherehe za kitaifa za Sikukuu ya Madaraka ambapo Makala ya 61 yaliandaliwa katika Kaunti ya Bungoma.

Katika mitandao ya kijamii, mwanafunzi huyo amekuwa akisifiwa jinsi alionyesha ukakamavu wake, ishara ya mtu anayejua anachotaka kuwa baadaye maishani.

Joy mwenyewe alielezea furaha yake kwa kuongoza kikosi hicho na akasema anatamani sana kukutana na Rais Ruto.

“Napenda kuongoza maskauti wenzangu. Natumai siku moja nitakutana na Rais Ruto na kumwambia vitu ninavyojua vinaweza kutusaidia kufanikiwa,” akasema Joy.

Mwanafunzi Joy Baraka (mbele) wa Bungoma DEB, msichana jasiri wa Gredi ya Tatu aliyesisimua wakati wa gwaride la maskauti ambapo walimtumbuiza Rais William Ruto katika uwanja wa Masinde Muliro-Kanduyi. PICHA | JESSE CHENGE

Mwalimu wake, Bw Emmanuel Wetangula alisema mwanafunzi huyo ni kielelezo cha uongozi bora.

“Joy ni mwanafunzi mwenye maono maishani,” akasema Bw Wetangula.

Mwalimu wake mwingine, Bi Judith Chebet, aliambia Taifa Leo kwamba Joy amewapa tabasamu hapo shuleni Bungoma DEB.

“Mwanafunzi wetu alionyesha moyo wa kujitolea unaohitajika kwa Mkenya yeyote mzalendo na viongozi,” akasema Bi Chebet.

Mkuu wa shule hiyo, Bw Tobias Khisa, alitoa wito kwa wadau kumsaidia Joy ili kukutana na Rais.

“Matumaini yangu ni kwamba atapata fursa ya kukutana na Rais siku moja,” akasema Bw Khisa.

Mwalimu mkuu wa Bungoma DEB Bw Tobias Khisa akiwa na mwanafunzi Joy Baraka. PICHA | JESSE CHENGE

Vilevile mwalimu mkuu huyo amemuomba Rais kuisaidia shule kupata basi.

Alisema shule hiyo huandikisha matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa na hufanya vyema katika michezo.

“Tukipata basi itakuwa rahisi kwa wanafunzi wetu kufika kwa urahisi maeneo tofauti kwa mashindano,” akasema.